Kuna ongezeko la hatari dhidi ya watoto CAR - UNICEF 

Kijiji cha Liton, katika mkoa wa Begoua, kaskazini mwa Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambapo wanaume, wanawake na watoto 2,000 wamekimbia vijiji vyao tangu mapigano ya Januari 2021 huko na karibu na PK12.
MINUSCA/Hervé Serefio
Kijiji cha Liton, katika mkoa wa Begoua, kaskazini mwa Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambapo wanaume, wanawake na watoto 2,000 wamekimbia vijiji vyao tangu mapigano ya Januari 2021 huko na karibu na PK12.

Kuna ongezeko la hatari dhidi ya watoto CAR - UNICEF 

Amani na Usalama

Mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, NCHINI Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Fran Equiza, hii leo akizungumza na wanahabari mjini Geneva Uswisi amesema, "watoto 370,000 kwa sasa ni wakimbizi wa ndani nchini kote kwa sababu ya vurugu zinazoendelea na ukosefu wa usalama. Hiki ni kiwango cha juu kabisa cha watoto kufurushwa katika makazi yao tangu 2014." 

Kiongozi huyo ameanza kwa kueleza kwamba kwa makadirio ya hivi karibuni, takribani watoto 168,000 walilazimishwa kukimbia nyumbani kwao kutokana na vurugu zilizotapakaa zikitokana na uchaguzi mkuu mwezi Desemba nchini CAR.  

Aidha Bwana Equiza amesema UNICEF inaonya juu ya hatari zinazozidi kuongezeka kwa watoto, pamoja na kuathiriwa na unyanyasaji wa kingono na mwili, kuajiriwa katika vikosi vya jeshi na makundi ya wapiganaji, kuongezeka kwa viwango vya utapiamlo na ufikiaji mdogo wa huduma muhimu. 

"Tuna wasiwasi sana juu ya hatima ya maelfu ya watoto ambao, baada ya kuona maisha yao yamegeuzwa chini juu na mizozo na vurugu, sasa wanaweza kupata kiwewe cha ziada kwa kulazimishwa kujiunga na kuishi kati ya watu wenye silaha, kushiriki katika vita, kuweka wote wawili na maisha ya wengine walio katika hatari kubwa. Asilimia 53 ya idadi ya watu, ambao nusu yao ni watoto, wanahitaji msaada wa kibinadamu.” Amesema Bwana Equiza.  

Vilevile Mwakilishi huyo wa UNICEF nchini CAR ameeleza kuwa, UNICEF inafanya kazi kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs ya kitaifa na ya kimataifa, au kwa kupeleka wafanyakazi wake kwa muda wakati hakuna washirika, kufikia watu wale wanaohitaji msaada wa kuokoa maisha, pamoja na afya, ulinzi, maji usafi wa mazingira, pamoja na elimu. 

Licha ya changamoto kubwa, pamoja na mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu, UNICEF inaendelea kuimarisha shughuli zake za ulinzi wa watoto kote CAR. Jitihada hizi ni pamoja na kupelekwa kwa timu za ulinzi wa watoto ambazo zinaweza kufikia watoto walio katika mazingira magumu, pamoja na zile zilizoko maeneo ya mbali. UNICEF na wadau wake pia wanafanya kazi ya kuwapa watoto afya ya akili na shughuli za kisaikolojia kupitia njia zinazofaa kwa watoto na hatua nyingine za kijamii.