Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yapita nyumba kwa nyumba ili kuwapatia chanjo ya COVID-19 wanaoishi vijiji vya ndani Colombia

Chanjo ya COVAX
© UNICEF Moldova
Chanjo ya COVAX

WHO yapita nyumba kwa nyumba ili kuwapatia chanjo ya COVID-19 wanaoishi vijiji vya ndani Colombia

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, kwa kushirikiana na mamlaka nchini Colombia wanatumia kila njia ikiwemo ya kutembea nyumba kwa nyumba ili kuwafikia watu wa jamii za asili walio katika mazingira magumu katika eneo la Amazon kusini mwa nchi ambao ni miongoni mwa makundi ya kipaumbele ya kupatiwa chanjo ya COVID-19.

 

Katika hospitali ya Inirida nchini Colombia, mratibu wa chanjo anaonekana akiandaa chanjo za coronavirus">COVID-19. Kisha anawakabidhi watakaoingia mitaani kuchanja watu. Chanjo zinahifadhiwa katika vibebeo vinavyozikinga na joto ambavyo ndani vimewekewa vipande vya barafu. Mara baada ya kila kitu kuwekwa katika nafasi yake, wahudumu wa afya wanapanda katika magari, tayari kuvuka vilima, mabonde, barabara mbovu na madaraja ya mbao ili kuzifikia jamii zilizoko ndani.  

Karibu na mji wa Inírida, timu za afya zimeanzisha kituo cha muda cha chanjo. Na ili kufikia idadi kubwa ya watu kwa haraka wanawatumia wahudumu wa afya wenyeji ili kuendana na tamaduni za wenyeji na pia wamebadili utaratibu wa kuchanja makundi fulani katika jamii.  Fabian Niño, ni Mratibu wa chanjo anasema, "wizara imelipa kipaumbele eneo hili kwa sababu ya maambukizi yaliyoko Brazil ambayo yako karibu kwa sababu tuna mpaka na Brazil. Kwa hivyo, wamesema: ‘Chanja watu wote zaidi ya umri wa miaka 18 katika mji wa Inírida." 

Inirida na maeneo jirani angalau ni mjini, lakini Paujil katika makazi yaliyoko kandoni mwa mto wanakoishi watu wa asili, timu za wahudumu wa afya, baada ya kuyakata mawimbi mtoni, wanaenda nyumba kwa nyumba ili kuwapa chanjo wakazi wengi wa jamii iwezekanavyo. Dkt Ivy Talavera ni mtaalam mshauri wa Familia, Jinsia na Maisha wa WHO anasema, "katika hali maalum ya watu wa Amazon, tunajua kwamba watu hawa wanaishi katika mazingira magumu. Tunao ugumu wa kuwafikia, kwa sababu ya jiografia, fursa zisizo sawa za kiuchumi na upatikanaji wa huduma usio na usawa. Na mambo haya yote ya kijamii yote vya kijamii yanachangia ufikiaji mdogo zaidi. Kuifanya huduma ipatikane inahitaji uimarishaji, sio tu kuhusu afya. Lazima iwe hatua zaidi ya afya tu, ili kutoa chanjo katika maeneo ya mbali. " 

Kufikia tarehe 5 ya mwezi huu wa Aprili, zaidi ya watu milioni 2.4 wamethibitishwa kupata maambukizi ya COVID-19 nchini Colombia, na kusababisha vifo takribani 64,000. Mamlaka za Colombia zinashughulikia changamoto ya kufikia jamii za asilii za vijijini, ambazo nyingine zinaweza kufikiwa tu kwa njia ya anga au mto. Dkt Ivy anaeleza namna hali ilivyo tofauti vijijini, "hatuwezi kufanya kazi hapa  kwa njia sawa na tunavyofanya katika mji. Kwa hivyo, tunapaswa kubadilisha hatua zetu. Kwa hivyo, ikiwa tuna watu, hasa watu wanaoishi katika hifadhi, watu wa asili, ni muhimu kutambua kuwa wana utofauti na wana mambo yao ya kitamaduni, sababu zao za kuishi ambazo zinawafanya wawe tofauti, lakini haimaanishi tofauti kwa jinsi ya kuchukua chanjo. Kwa hivyo, mambo haya ya kitamaduni ni muhimu kuzingatia ili kuwa na uwezekano wa kuwa pia wanapata chanjo salama.” 

Kisha Dkt Talavera anaongeza, akisema, “hapo unakuja mchakato muhimu ambao ni mawasiliano. Je! Ujumbe unasambazwaje ili uweze kukubalika na watu tofauti: mawasiliano kuhusu hatari, usalama wa chanjo, jinsi ya kufikisha ujumbe kwa kiwango cha lugha zao na utaalam wao wenyewe, kuelewa upotofu wa taarifa katika watu. Jinsi wanavyofikiria, jinsi wanavyotafsiri mchakato wa ugonjwa. Mambo hayo ya asili na  uumbaji na tabia ya wenyeji vinapaswa kuzingatiwa. " 

COVAX, nguzo ya mkakati wa kimataifa wa kukabiliana na COVID-19 ACT, inaongozwa kwa ushirikiano wa  Ushirika wa ubunifu wa maandalizi dhidi ya milipuko ya magonjwa ,CEPI, Muungano wa Chanjo, Gavi na WHO kwa kushirikiana na wazalishaji wa chanjo wa nchi zilizoendelea na zinazoendelea, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la afya la nchi za Amerika PAHO, Benki ya Dunia, na ningine. Ni mpango pekee wa ulimwengu ambao unafanya kazi na serikali na watengenezaji kuhakikisha chanjo za COVID-19 zinapatikana ulimwenguni kote kwa nchi zenye kipato cha juu na kipato cha chini.