Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika jiandae na ongezeko kubwa la wagonjwa wapya wa COVID-19- WHO

Eunice Marorongwe amepona ugonjwa wa COVID-19 na kurejea kazini kuwasaidia wagonjwa
© UNICEF
Eunice Marorongwe amepona ugonjwa wa COVID-19 na kurejea kazini kuwasaidia wagonjwa

Afrika jiandae na ongezeko kubwa la wagonjwa wapya wa COVID-19- WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO hii leo limesema Afrika imekuwa na wiki mbaya zaidi ya mapambano ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, ambayo haijawahi kutokea. Pia imeonya hali mbaya zaidi inakuja, kwani kutakuwa na ongezeko kubwa na kwa kasi ndani ya wiki chache zijazo. 

Idadi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19 imeendelea kupanda kwa wiki saba mfulilizo tangu kuanza kwa awamu ya tatu ya janga hilo mwezi Mei mwaka huu wa 2021. Kwa wiki iliyoishia na tarehe 4 mwezi huu wa Julai, zaidi ya wagonjwa wapya 251,000 wamerekodiwa ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na wiki iliyopita.

“Bara la Afrika limeshuhudia wiki mbaya ya janga la Corona. Lakini hali mbaya zaidi inakuja katika wimbi hili la tatu ambalo maambukizi mapya yanaendelea kupanda katika uwanja mpya kabisa” amesema Dkt. Motshidiso Moeti Mkurugenzi wa WHO kanda ya ya Afrika. 

Dkt. Moeti ameongeza kuwa “mwisho wa kuongezeka kwa maambukizi haya bado sana, wiki nyingi bado tutaendelea kushuhudia maambukizi. Wagonjwa wanaongezeka maradufu kila baada ya siku 18, ikilinganishwa na kila siku 21 hapo wiki iliyopita. Bado tunaweza kuvunja mnyororo huu wa maambukizi kwa kupima, kuwatenganisha waliochangamana na waliogundulika kuwa na maambukizi,na kufuata masharti muhimu yanayotolewa na wahudumu wa afya kwa umma. “

Kuhusiana na chanjo ndani ya bara la Afrika kwani awali takwimu zilionesha ni asilimia 1 tu ndio wamepata chanjo, WHO imesema imeona maendeleo chanya kwenye upatikanaji wa chanjo ambapo mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuchagiza upatikanaji wa chanjo COVAX kwa nchi za kipato cha chini umeshika kasi katika kuzisambaza Afrika. Ndani ya wiki mbili, zaidi ya dozi milioni 1.6 zilisambazwa na ongezeko la dozi milioni 20 zinatarajiwa kufika hivi karibuni ikiwa ni msaada wa Marekani kupitia COVAX

 

Umoja wa Mataifa umesaidia kampeni za kuelimisha wananchi vijijini kuhusu janga la COVID-19
WFP/Badre Bahaji
Umoja wa Mataifa umesaidia kampeni za kuelimisha wananchi vijijini kuhusu janga la COVID-19

  Hali ya COVID-19 nchini Malawi  

Nchini Malawi Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo Maria Jose Torres Macho anaongoza timu inayoshirikiana na serikali ya Malawi kukabiliana na changamoto kadhaa zilizotokana na janga la Corona. 

Wagonjwa wa COVID-19 wameongezeka kwa kasi katika miezi ya hivi karibuni na serikali imepiga marufuku safari na mikusanyiko ya wazi il kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Kuhusiana na uhaba wa chanjo, mashirika ya Umoja wa Mataifa ya WHO na UNICEF wanashughulikia uingizwaji nchini humo wa chanjo 900,000 kupitia COVAX. Mashirika hayo pia yanaisaidia serikali ya Malawi katika kuwafanyia uchunguzi wasafiri, kupima na kuchunguza wale wote waliokutana na wagonjwa wa COVID-19 waliotambulika. 

Mpaka sasa, zaidi ya vifaa vya kupimia 10,000 vimeshatolewa. Timu ya Umoja wa Mataifa pia inashirika katika kampeni ya kuelimisha umma jinsi ya kujilinda wasipate maambukizi.

Pia wametoa fedha kwa zaidi ya wananchi 100,000 ikiwa ni kuwasaidia kukabiliana na atthari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la Corona.