Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Muuguzia nchini Ghana akimchoma mwanamke chanjo ya Corona

Benki ya Dunia yaingilia kati kukabili uhaba wa chanjo Afrika

© UNICEF/Apagnawen Annankra
Muuguzia nchini Ghana akimchoma mwanamke chanjo ya Corona

Benki ya Dunia yaingilia kati kukabili uhaba wa chanjo Afrika

Afya

Katika kufanikisha lengo la Muungano wa Afrika, AU kuhakikisha asilimia 60 ya wakazi wa bara lake wamepatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 ifikapo mwaka 2022, Benki ya Dunia na AU wametangaza ubia wa kuunga mkono mpango wa kikosi kazi cha Afrika cha kupata chanjo hizo, AVATT utakaoruhusu nchi za Afrika kununua na kusambaza dozi za chanjo kwa ajli ya watu milioni 400 barani kote.

Makubalinao yamekuja baada ya mkutano kati ya Benki ya Dunia na Mawaziri wa Fedha wa Afrika na hatua hiyo naenda kuunga mkono ile ya kimataifa ya COVAX wakati huu ambapo kuna ongezeko la wagonjwa wa Corona barani Afrika. 
Mkurugenzi wa Operesheni katika Benki ya Dunia Axel Trotsenburg amesema lengo ni kuzuia mlipuko wa tatu wa COVID-19 na kwamba, “Tumeshirikiana pamoja kuhusu  mkataba uliofikiwa kati ya Muungano wa Afrika na kampuni  ya Johnson And Johnson wa kusambaza dozi milioni 400 za chanjo barani Afrika chanjo ambazo mtu anapata dozi moja. Hizi chanjo zinahitaij ufadhili na hapo Benki ya Dunia ndipo inaingia kwa kutoa fedha zote.” 

Mkurugenzi huyo akafafanua kwa nini ni muhimu hivi sasa kusaidia bara la Afrika. “Ni takwimu moja tu: Hadi leo hii, wakazi wa Afrika waliopatiwa chanjo ni chini ya asilimia Moja. Afrika imeenguliwa katika juhudi za kimataifa za kupata chanjo . Lazima turekebishe hali hii ya ukosefu wa haki. Na kwa kutambua kuwa hili ni janga la dunia, tunahitaji suluhu za kimataifa na mshikamano wa kimataifa, hauwezi kuliacha bara la Afrika kwenye uzingatiaji huu.” 

Benki ya Dunia ina dola bilioni 12 za kusaidia nchi kununua na kusambaza chanjo ambapo tayari imeshaidhiisha operesheni za kusaidia chanjo  ya COVID-19 katika mataifa 36. Lengo lake sasa ni kuhakikisha kuwa hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Juni, iwe imesaidia nchi 50 duniani ambapo theluthi mbili ziko Afrika.