Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunapojikwamua kutoka COVID-19 tusisahau watu wenye usonji- Guterres

Clara Lopez Baro akiwa na mwanae Jonathan Alvarez Lopez nyumbani kwao Havana nchini Cuba, ambako wamelazimika kukaa ndani kutokana na COVID-19
UNICEF Cuba
Clara Lopez Baro akiwa na mwanae Jonathan Alvarez Lopez nyumbani kwao Havana nchini Cuba, ambako wamelazimika kukaa ndani kutokana na COVID-19

Tunapojikwamua kutoka COVID-19 tusisahau watu wenye usonji- Guterres

Afya

leo  ni siku ya usonji duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka harakati zozote za kujikwamua kutoka katika janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 ni lazima zilenge kujenga dunia inayotambua mchango wa watu wote wakiwemo watu wenye ulemavu.
 

Guterres katika ujumbe wake wa siku hii leo, amesema, “janga la Corona limejenga vikwazo na changamoto mpya. Lakini juhudi za kuchechemua uchumi wa dunia zinatoa fursa mpya ya kutazama upya mahala pa kazi na kuhakikisha panakuwa jumuishi, pana watu wa aina tofauti, na pana uwiano na usawa.”

Katibu Mkuu amesema kujukwamua pia ni fursa ya kufikiria upya kuhusu mifumo ya elimu na mafunzo ili kuhakikisha watu wenye usonji nao wanapatiwa fursa ya kufikia ustawi wao.

Soundcloud

Hata hivyo amesema kuondokana na tabia za zamani, “kwa watu wenye usonji, kupata ajira zenye utu kwa usawa kunahitaji mazingira wezeshi, sambamba na malazi bora. Na hakika ili kutomwacha mtu yeyote nyuma katika kufanikisha ajenda 2030 au malengo ya maendeleo endelevu, tunapaswa kufanikisha haki za watu wenye ulemavu, wakiwemo watu wenye usonji, kuhakikisha wanashiriki kikamilifu maisha yao kijamii, kitamaduni na kiuchumi.”

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaka ushirikiano na watu wote wenye ulemavu sambamba na mashirika yanayowawakilisha ili hatimaye kuwa na suluhu bunifu za kujikwamua vyema kutoka katika janga na kuwa na dunia bora kwa kila mtu.

Ugonjwa wa Usonji kwa kiingereza Autism, ni ugonjwa ambao kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO  hukumba mtoto mmoja kati ya kila watoto 160 duniani. Usonji ni tatizo la kibaiolojia analopata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake na dalili huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea na mtoto akiwa na tatizo hilo kasi yake ya kukua kiakili inakuwa ndogo kulingana na kasi ya kukua kimwili.

Kabla ya hapo wataalamu wanasema ni aghalabu kuona dalili hizo ambapo zinapojitokeza mtoto hukosa mbinu za uhusiano, anashindwa kuzungumza na wakati mwingine kurukaruka na hata kujing’ata. Watoto hawa kutokana na tatizo hilo wengine hutekelezwa na jamii na kunyimwa haki zao za msingi ikiwemo kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa