Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Siku ya kujenga uelewa kuhusu Usonji huadhimishwa tarehe 02 Aprili kila mwaka

Ili kutimiza lengo la kutomwacha yeyote nyuma lazima tuwajumuishe watu wenye usonji:Guterres

UNSPLASH/Michal Parzuchowski
Siku ya kujenga uelewa kuhusu Usonji huadhimishwa tarehe 02 Aprili kila mwaka

Ili kutimiza lengo la kutomwacha yeyote nyuma lazima tuwajumuishe watu wenye usonji:Guterres

Haki za binadamu

Leo ni siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu usonji na Umoja wa Mataifa unasisitiza haja ya kuwajumuisha watu wenye ulemavu ikiwemo wenye usonji ili kutimiza azma ya Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ya kutomuacha yeyote nyuma. 

Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Tunapofanya kazi pamoja ili kujikwamua kutokana na janga la COVID-19, lengo moja kuu lazima liwe kujenga ulimwengu unaojumuisha watu wote na unaoweza kufikiwa ambao unatambua michango ya watu wote, wakiwemo watu wenye ulemavu.” 

Guterres amesema janga hili la COVID-19 limezua vikwazo na changamoto mpya.  

Lakini juhudi za kufufua uchumi wa dunia zinatoa fursa ya kufikiria upya mahali pa kazi ili kuleta tofauti, ushirikishwaji na usawa kuwa hali halizi.

Mtoto mdogo aliye na usonji akicheza kwenye uwanja wa michezo wa shule ya Alpha Learners with Autism huko Cape Town, Afrika Kusini.
© UNICEF/Brian Sokol
Mtoto mdogo aliye na usonji akicheza kwenye uwanja wa michezo wa shule ya Alpha Learners with Autism huko Cape Town, Afrika Kusini.

Ameongeza kuwa “Kujikwamua huko pia ni nafasi ya kutafakari upya mifumo yetu ya elimu na mafunzo ili kuhakikisha kuwa watu walio na usonji wanapewa fursa za kufikia uwezo wao.” 
 
Pia amesisitiza kwamba “Kuacha mazoea ya zamani itakuwa muhimu. Kwa watu walio na usonji, upatikanaji wa kazi zenye staha kwa misingi sawa unahitaji kuunda mazingira wezeshi, pamoja na malazi ya kuridhisha.” 

Na zaidi ya hayo amehimiza kuwa “Ili kweli tusimwache mtu yeyote nyuma katika kutekeleza ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu, ni lazima tutambue haki za watu wote wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na watu wenye usonji, kuhakikisha ushiriki wao kamili katika maisha ya kijamii, kiutamaduni na kiuchumi.” 

Kwa mantiki hiyo amesema “Hebu tufanye kazi pamoja na watu wote wenye ulemavu na mashirika yanayowawakilisha ili kupata suluhu za kibunifu ili kujikwamua vyema na kujenga ulimwengu bora kwa wote.”