Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya kuishi na watoto wenye usonji yaleta manufaa kwa wazazi 

Mafunzo kwa mtoto mwenye usonji.
UNICEF
Mafunzo kwa mtoto mwenye usonji.

Mafunzo ya kuishi na watoto wenye usonji yaleta manufaa kwa wazazi 

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO kwa kushirikiana na shirika la PANAACEA wanatoa mafunzo nchini Argentina ya kuwezesha watoto wenye usonji kukabiliana na changamoto za ulemavu zinazowakabili ikiwemo kuchelewa kuzungumza.

Nchini Argentina, mtoto Gabriel na nduguze wawili wakicheza mezani wakiwa na mama  yao. 

Gabriel alibainika kuwa na usonji akiwa na umri wa miaka mitatu, wakati huo hawezi kuzungumza wala kushirikiana na familia yake. 

Ingawa hivyo mama yake mwenye watoto wanne alilazimika kumpatia msaada anaohitaji. 

Alisaka msaada wa tiba ya usonji na alielekezwa kupata mafunzo stadi ya malezi au CST yanayoendeshwa na WHO kwa ubia na PANAACEA. 

 “Ilikuwa vigumu , kipindi kile kuwasiliana na mwanangu . nilikuwa sijui nifanyaje. Na programu hii imenionesha kuna njia, ninachotakiwa tuu ni kujifunza namna ya kumfikia”.  Amesema Karina Visciglia mama yake Gabriel. 

Programu hii inayolenga kusaidia familia za watoto wenye matatizo ya kukua, kuzungumza au ulemavu mwingine ikiwemo usonji hutoa mafunzo ya malezi ya familia. Wakufunzi si wataalamu bali wafanyakazi wa kijamii wenye watoto walio na matatizo kama hayo. 

Dkt.Sebastian Cukier mwanasaikolojia ya watoto na vijana ambaye pia ni mwanzilishi mwenza wa programu ya PANAACEA anasema, 

“Mtoto akiwa na tatizo, mzazi anakuwa anategemea wataalamu. Hii programu inamuwezesha mzazi kutoa muongozo kwa mtoto wake, kuwa na uhusiano mzuri na mtoto wake na mawasiliano” 

Mafunzo ni kwa njia ya vikundi na hutembelea majumbani ambapo pia wakufunzi wanapata fursa ya kushuhudia maendeleo. 

Pia wanafundishwa jinsi ya kuwasiliana, kushirikiana, stadi za maisha, mazingira magumu na namna ya kukabiliana nayo.Natalia Barrios ni mkufunzi CST. 

“Tunapowatembelea majumbani, tunaangalia namna wazazi wanavyotumia mbinu tulizowafundisha na kuwaelimisha namna ya kuboresha mawasiliano zaidi na kufuata mbinu ambazo hawakuwea kuzifuata vizuri.” 

Mama yake Gabriel anakiri kuona mabadiliko,“Alikuwa katika ulimwengu mwingine kabisa. Lakini sasa mwanangu yupo hapa na tunawasiliana. Anaajitahidi kuhakikisha watu wanamsikiliza. Anaeleza maamuzi yake na kuwafanya watu wayaheshimu. Kitu anachokitaka, kitu anachohisi. Hii imewezekana kutokana na programu hii “ 

Kuibuka kwa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 kulilazimu wakufunzi kuendesha mafunzo kimtandao badala ya kufanya ziara majumbani.