Janga la COVID-19 linawaweka watu wenye usonji katika hatari kubwa.

Janga la COVID-19 linawaweka watu wenye usonji katika hatari kubwa.
Kupitia ujumbe wake maalum kwa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema siku ya uelimishaji kuhusu usonji inaadhimishwa kwa kutambua na kusherehekea haki za watu wenye usoni na kwamba “Mwaka huu siku hii inaadhimishwa katikati ya janga la kimataifa la kiafya ambalo hatujawahi kulishuhudia katika maisha yetu, janga ambalo linawaweka watu wenye usonji katika hatari kubwa kutokana na virusi vya Corona na athari zake katika jamii.”
Guterres ameongeza kuwa “watu wenye usonji wana haki ya kufanya maamuzi, kuwa huru na kujitawala pamoja na haki ya elimu na ajira saw ana wengine. Lakini kuvurugika kwa mfumo na mitandao ya msaada kutokana na virusi vya corona, COVID-19 kumezidisha vikwazo ambavyo watu wenye usonji wanakumbana navyo katika kutekeleza haki zao.”
Katibu Mkuu amesisitiza ni lazima kuhakikisha kwamba usumbufu wa muda mrefu uliosababishwa na dharura ya janga hili hakuchangii kurudisha nyuma haki za watu wenye usonji ambazo mashirika yanayowawakilisha yamefanya kazi kubwa kuzifikia.
Ukurasa kuhusu virusivyacorona & taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.Amekumbusha kwamba “haki za kimataifa za binadamu zikiwemo za watu wenye ulemavu haipaswi kukiukwa wakati huu wa COVIDI-19. Serikali zinawajibu wa kuhakikisha hatua zao zinajumuisha watu wenye usonji. Watu wenye usonji hawapaswi kukabiliwa na ubaguzi wakati wanaosaka huduma za afya. Wanastahili kuendelea kuwa na fursa ya mfumo wa msaada unaohitajika ili waweze kusalia majumbani kwao na katikajamii zao wakati wa janga, badala ya kukabiliwa na matarajio ya kulazimishwa kusalia kwenye vituo.”
Bwana Guterres ameongeza kuwa kila mmoja ana jukumu la kufanya kuhakikisha mahitaji ya watu wanaoathirika zaidi na COVID-19 yanatimizwa katika kipindi hiki kigumu. Pia ameasa kwamba taarifa kuhusu hatua za kujikinga zinapaswa kufikishwa kwa njia ambayo inaweza kuwafikia kwa urahisi.
"Pia ni lazima tutambue kwamba wakati shule zinapofundishwa kwa njia ya mtandao, wanafunzi wasio na njia za kujifunza wanaweza kuwa katika wakati mgumu na hiyo ni pamoja na maeneo ya kazi na kufanyia kazi nje ya mazingra ya kazi.”
Katibu Mkuu amesema hata katika nyakati hizi zisizotabirika ni lazima tuahidi kuwasiliana na watu wenye ulemavu na mashirika yanayowawakilisha na kuhakikisha kwamba njia zetu ambazo si za asili za kufanya kazi, kusoma na kujihusisha na wengine pamoja na jududi za kimataifa za kukabiliana na virusi vya corona ni jumuishi na zinapatikana kwa watu wote wakiwemo wenye usonji.
Haki za watu wenye usonji ni lazima zizingatiwe katika kuandaa mikakati na hatua zote za kukabiliana na virusi vya COVID-19.
“Katika siku hii ya uelimishaji kuhusu usonji duniani hebu tusimame pamoja , tusaidiane na kuonyesha mshikamano na watu wenye usonji.”
Kaulimbiu ya siku ya usonji mwaka huu ambayo kila mwaka huadhimishwa Aprili 2 ni “kuelekea utu uzima”.