Skip to main content

Watu 1,600 wamechanjwa dhidi ya Ebola Guinea, chanjo zaidi zahitajika: WHO

Chanjo ya Ebola yaanza nchini Guinea ili kuzuia mlipuko mpya.
WHO
Chanjo ya Ebola yaanza nchini Guinea ili kuzuia mlipuko mpya.

Watu 1,600 wamechanjwa dhidi ya Ebola Guinea, chanjo zaidi zahitajika: WHO

Afya

Watu zaidi ya 1,600 wameshapokea chanjo dhidi ya virusi hatari vya Ebola ambako shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linasema watu wanne wamepoteza maisha kufuatia mlipuko mpya wa ugonjwa.

Kupitia taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis chanjo zaiodi zinahitajika ili kuudhibiti mlipuko huo.

Hadi kufikia sasa, visa 18 vya Ebola vimeripotiwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi , wagonjwa 14 wamethibitishwa na vifo vine.

 Chanjo 30,000 tu za Ebola ndizo zimepatikana, nkati ya hisa ya kimataifa ya chanjo nusu milioni.

"Tunatumia chanjo ya mzunguko," amesema Dkt. Ibrahima Socé Fall, Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa WHO anayehusika na hatua za dharura, akimaanisha mkakati ambao unazuia kuenea kwa ugonjwa kwa kutoa chanjo tu wale ambao wanaoweza kuambukizwa.

“Tunawachanja watu waliokutana na wagonjwa, na wale walookutana na hao, na waliokutana na hao pia. Kwa mkakati huu tunaweza kudhibiti aina hii ya mlipuko. Lakini tutahitaji chanjo zaidi, ”Dkt. Fall amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva.

Akina ndogo ya chanjo

 

"Ikiwa mlipuko utaenea kwa nchi zingine, tuna akiba ndogo sana ya chanjo" amesema Mkurugenzi wa operesheni ya Afya ya kimkakati katika shirika la WHO, Dkt. Michel Yao akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa Habari kwa njia ya video kutoka mji wa Nzérékoré nchini Guinea, moja ya kitovu cha mlipuko huo, karibu na mpaka na Liberia na Côte d'Ivoire.

 Mlipuko wa mwisho wa Ebola nchini Guinea, ambao ulianza mnamo 2014, ulienea haraka hadi nchi jirani za Liberia na Sierra Leone. 

Wakati ulipodhibitiwa, ulikuwa ni mlipuko mbaya zaidi wa Ebola tangu virusi vigunduliwe kwa mara ya kwanza mwaka 1976, ukiwa na jumla ya wagonjwa 28,000 na vifo 11,000. 

 Utayari mpakani

"Kuna nchi sita jirani na Guinea, na tulifanya tathmini binafsi ya utayari," amesema Gueye Abdou Salam, mkurugenzi wa dharura wa WHO kanda ya Afrika, akizungumza kutoka Brazzaville. 

Ameongeza kuwa "Nchi mbili haziko tayari, na nchi moja iko kwenye hatihati na kuna nchi tatu ambazo ama ziko tayari au zimejiandaa kidogo."

Wataalam wanasema baada ya kukabiliwa na milipuko ya awali ya Ebola hii imeipa mamlaka ya afya faida kubwa wakati huu.

"Ni muhimu kujifunza kutokana na milipuko hii," amesema Dakt. Georges Alfred Ki-Zerbo, mwakilishi wa WHO nchini Guinea, ambaye aliangazia hitaji la kupata imani kwa jamii za wenyeji katika maeneo yote ambayo kampeni za chanjo zilipangwa kufanyika.

"Ambako tunazindua kampeni ya chanjo huko Gouecke, kilomita chache kutoka hapo kuna kijiji cha Wome. Hapa ndipo timu ya maafisa na wahudumu wa afya walikwama na kupoteza maisha katika mlipuko wa mwisho mnamo 2015. Kwa hivyo, tunahitaji kuzingatia wakati tunaposhirikiana na jamii kuhakikisha kuwa tunawasikiliza, ” amesema Dk Ki-Zerbo.

Mlipuko wa ebola umeripotiwa nchini Guinea. (Maktaba)
WHO/Junior D. Kannah
Mlipuko wa ebola umeripotiwa nchini Guinea. (Maktaba)

Vimelea vinavyoua

Kuna makubaliano makubwa miongoni mwa maafisa wa afya kwamba kuchukua hatua haraka ni jambo muhimu katika kudhibiti kuenea kwa Ebola, lakini hatua za kinga na maandalizi bora pia vinahitajika ili kulinda watu dhidi ya vimelea vya magonjwa mbalimbali.

Dr Fall amesisitiza kwamba ulimwengu utakabiliwa na idadi kubwa ya magonjwa ya milipuko ya kiafya, hususan  ambapo makazi ya wanadamu yanapoingilia maeneo ya misitu.

"Tunazidi kuwa katika hali ambayo tunalazimika kukabiliwa na magonjwa mengi ya milipuko. Nchi lazima ziwezeshwe kukabili magonjwa mengi yamlipuko, lakini haswa ni kupitia njia za kinga." Ameongherza Dkt. Fall

Changamoto moja ya sasa ni kwamba kuzingatia zaidi janga la COVID-19 inafanya kuwa ngumu zaidi kuelekeza umakini wa ulimwengu kwenye zana zinazohitajika kukabiliana na vimelea vingine vyovyote vinavyoibuka.