Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko DRC yanatishia mustakbali wa watoto milioni 3 waliotawanywa : UNICEF

Ukatili wa vikundi vilivyojihami unatishia maisha ya watoto milioni 3 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.
© UNICEF/Roger LeMoyne
Ukatili wa vikundi vilivyojihami unatishia maisha ya watoto milioni 3 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Machafuko DRC yanatishia mustakbali wa watoto milioni 3 waliotawanywa : UNICEF

Amani na Usalama

 Maisha na mustakbali wa watoto zaidi ya milioni 3 waliotawanywa nchini Jasmhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, uko hatari huku dunia ikiwapa kisogo  kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Ripoti hiyo imesema “Mashariki mwa DRC kuendelea kwa mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na wapiganaji kwa kutumia mapanga na silaha nzitonzito kumezilazimisha jamii zote kukimbia na kuacha kila kitu huku familia wakiwemo watoto wametekwa hadi kuuawa, vituo vya afya na shule vimeporwa na vijiji vyote kuchomwa moto.” 

Ripoti imetoa wito wa kukomeshwa kwa machafuko ambayo yamechochea kuwa na moja ya mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani. 

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba hivi sasa kuna watu milioni 5.2 waliotawanywa nchini DRC wakiwa ni wengi kuliko nchi nyingine yoyote isipokuwa Syria na asilimia 50 kati ya watu hao wametawanywa katika miezi 12 iliyopita pekee. 

Mazingira wanayoishi waliotawanywa 

 

Kwa mujibu wa ripoti familia zilizotawanywa zinaishi katika makazi yaliyo na msongamano ambayo yanakosa maji salama, huduma za afya na huduma zingine za msingi. 

Watu wengine wanahifadhiwa katika jamii ambazo pia ni masikini na katika majimbo yaliyoathirika sana na machafuko ya Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Tanganyika zaidi ya watu milioni 8 wanakabiliwa na hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula. 

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Edouard Beigbeder amesema “Watoto waliotawanywa hawana wanalolijua isipokuwa hofu, umasikini na vita. Kizazi hata kizazi watakachokuwa wanakiwaza ni jinsi ya kunuru Maisha yao. Laskini bado dunia inalitazama vinginevyo janga hili na hatama ya Watoto hawa. Tunahitaji rasilimali ili kuendelea kuwasaidia watoto hawa ili wawe na mustakabali bora.” 

Hali halisi inayowakabili watoto 

 

Ripoti hiyo inatanabaisha ushuhuda wa Watoto ambao wameajiriwa kama wapiganaji wa wanamgambo ambapo wengi wakinyanyaswa kingono na kupitia ukiukwaji mwingine mkubwa wa haki zao na ukiukwaji hyuo umetajwa kuongezeka kwa asilimia 16 katika miezi sita ya kwanza yam waka 2020 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. 

Kufikisha misaada ya kibinadamu kwa watu ambao wamekimbia makazi yao ni changamoto kubwa na mara nyingi huduma hiyo hukabniliwa na ukosefu wa usalama na miundombinu duni. 

Programu ya dharura inayoratibiwa na UNICEF na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali NGOs inlitoa suluhu ya muda kwa kugawa maturubai, vyombo vya kupikia, madumu ya maji na vitu vingine muhimu kwa karibu watu 500,000 mwaka 2020. 

“Hatua hizi za dharura zinasaidia kukabiliana na mshtuko wa kutawanywa lakini pia ni sehemu yah atua jumuishi zinazoangalia kushughulikia mahitafi makubwa ya familia katika suala la afya, lishe, ulinzi, huduma za WASH na elimu.” Amesema mkuu wa masuala ya dharura wa UNICEF nchini DRC Typhaine Gendron.  

Ripoti imekumbusha kwamba usalama ni mtihani mkubwa kwa wafanyakazi wa UNICEF, na washirika wao wa kitaifa na kimataifa. 

Kinachohitajika kufanywa 

 

Kwa mujibu wa ripoti kuendelea juhudi zilizopigwa kukabiliana na changamoto hizo ni suala la msingi na mshikamano wa kjumuiya ya kimataifa unajukumu kubwa. 

Walakini mshikamano huo wa jumuiya ya kimataifa na DRC hadi sasa unaonyesha kugonga mwamba kwani ombi la UNICEF la dola milioni 384.4 kwa ajili ya kusaidia masuala ya kibinadamu kwa mwaka 2021 hadi sasa limefadhiliwa kwa asilimia 11 pekee. 

“Bila uingiliaji endelevu wa hatua za msaada wa kibinadamu, maelfu ya watoto watakufa kutokana na utapiamlo au magonjwa na watu waliofurushwa makwao hawatapokea huduma muhimu za kuokoa Maisha wanazozitegemea” amesema Bwana. Beigbeder.