Maelfu ya watoto waendelea kuwa hatarini Ituri DRC:UNICEF 

6 Oktoba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limesema linaendelea kutiwa hofu kubwa kuhusu maelfu ya watoto walio hatarini wakati huu machafuko yakiendelea kwenye jimbo la Ituri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo watoto wanaendelea kuteseka kwa sababu ya machafuko na vurugu zilizosababishwa na vita vya muda mrefu katika jimbo hilo.

UNICEF inasema machafuko yalishika kasi mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020 na tangu hapo hali kwa maelfu ya Watoto jimboni Ituri imezidi kuzorota. 

“Mashambulizi ya wanamgambo katika maeneo ya raia yamesababisha mamia ya vifo na UNICEF imepokea taarifa za watoto kujeruhiwa, kuawa au kuingizwa kwenye mapigano na makundi yenye silaha.Wakati huohuo zaidi ya watu milioni 1.6 wengi wao wakiwa ni wanawake na Watoto wanakadiriwa kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mchafuko hayo.” 

 

Athari za machafuko hayo 

 

Kwa mujibu wa UNICEF kati ya Januari na Juni 2020, watoto 91 wameuawa, 27 kujeruhiwa na 13 ni waathirika wa ukatili wa kingono. 

Pia karibu vituo 18 vya afya vimeporwa au kuharibiwa wakati mashambulizi dhidi ya shule 60 yamewaacha Watoto takriban 45,000 bila madarasa. 

Haya ni matukio yaliyothibitishwa lakini idfadi kamili huenda ikawa kubwa zaidi. Limesema shirika la UNICEF. 

Jimboni Ituri shirika hilo linasema hivi sasa kuna watu milioni 2.4 wanaohitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.  

Watu 150,000 wakiwemo Watoto 87,000 wamepatiwa msaada na UNICED na washirika wake hasa katika masuala ya huduma za afya na lishe, ulinzi, elimu, maji na usafi kati ya Januari na Agosti mwaka huu. 

 

Msaada mwingine uliotolewa  

 

Zaidi yah apo UNICEF na washirika wake pia wamewasaidia Watoto 365 ambao awali walikuwa wakihushwa na makundi ya wanagambo na yenye silaha kuweza kurejea na kujumuishwa katika jamii, kuwasafa ndugu wa familia zao na kuwapa msaada wa kisaikolojia. 

Watoto wengine 87,000 walio hatarini wamepewa fursa ya maeneo ya jamii ambako wanaweza kucheza na kujifunza. 

Kwa Watoto 68 waathirika wa ukatili wa kingono UNICEF imehakikisha wamepatiwa huduma za afya na msaada wa kisaikolojia na kisheria. 

Na kwa waathirika wengine 140,000 wa machafuko yanayoendelea wakiwemo Watoto 85,000 wanaendelea kupokea msaada wa vifaa ambavyo si chakula, malazi na vifaa vya usafi na kujisafi. 

Hata hivyo UNICEF imesema usalama mdogo kwenye jimbo la Ituri na ukata wa fedha vimeendelea kuathiri shughuli za misaada , huku ombi la UNICEF la dola milioni 318 lina pengo la asilimia 74 ambayo ni saw ana dola milioni 235. 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud