Mashambulizi dhidi ya walinda amani Mali yanaweza kuwa uhalifu wa kivita

13 Februari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mashambulizi dhidi ya walinda amani wa chombo hicho huko nchini Mali yanaweza kuwa  uhalifu wa kivita.
 

Bwana Guterres amesema hayo leo kupitia taarifa ya msemaji wake iliyotolewa jijini New York Marekani kufuatia ripoti ya kwamba mlinda amani mmoja aliyejeruhiwa katika shambulio huko Kerena jimbo la Douentza nchini Mali tarehe 10 mwezi huu amefariki dunia.

Mlinda amani huyo kutoka Togo alikuwa miongoni mwa walinda amani 28 wa Umoja wa Mataifa waliojeruhiwa baada ya watu wasiojulikana wakiwa na silaha kushambulia kituo cha muda cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSCA.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mlinda amani huyo pamoja na wananchi na serikali ya Togo. Halikadhalika amewatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Pamoja na kusema kuwa shambulio dhidi ya walinda amani linaweza kuwa uhalifu wa kivita, Bwana Guterres ametoa wito kwa mamlaka nchini Mali kufanya juhudi zote kusaka watekelezaji wa shambuli hilo la kikatili na wafikishwe mbele ya sheria.

Halikadhali amesisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na wananchi na serikali ya Mali.

Baraza la Usalama nalo lapaza sauti

Wakati huo hou, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulio hilo wakituma salamu za rambirambi kwa familia ya mlinda amani, wananchi na serikali ya Togo na wakiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Wamesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani yanaweza kuwa uhalifu wa kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kwamba upangaji, ufadhili, uongozaji au utekelezaji wa mashambulizi dhidi ya walinda amani wa MINUSMA unaweza kuwa msingi wa vikwazo kwa mujibu wa maazimio ya Baraza hilo.

Wajumbe wamesema kuwa ugaidi katika aina zozote zile ni moja ya vitisho vikuu vya amani na usalama duniani.
Wajumbe hao wamesisitiza uungaji mkono wao kwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali na Mkuu wa MINUSMA, Mahamat Saleh Annadif, MINUSMA na vikundi vingine vya usalama vilivyoko Mali na ukanda wa Sahel kama vilivyotajwa kwenye azimio namba 2531 la mwaka 2020 la Baraza la Usalama. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter