Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi ya walinda amani Mali yashambuliwa, walinda amani 20 wajeruhiwa

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali akiwa kwenye doria eneo la Mopti katikati mwa taifa hilo la Afrika Magharibi
MINUSMA/Gema Cortes
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali akiwa kwenye doria eneo la Mopti katikati mwa taifa hilo la Afrika Magharibi

Kambi ya walinda amani Mali yashambuliwa, walinda amani 20 wajeruhiwa

Amani na Usalama

Hii leo asubuhi kwa saa za Mali, magharibi wa Afrika, walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye kikosi cha kuweka utulivu nchini humo, MINUSMA wamedhibiti shambulio dhidi ya kituo chao cha muda cha Kéréna kilichopo maeneo ya Douentza katikati mwa Mali.
 

Taarifa ya MINUSMA iliyotolewa leo kwenye mji mkuu wa Mali, Bamako, imesema walinda amani waliweza kukabili washambuliaji ambao hatimaye walikimbia, ingawa walinda amani wapatao 20 walijeruhiwa.

Mwakilishi Maaalum wa  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali ambaye pia ni Mkuu wa MINUSMA, Mahamat Saleh Annadif amelaani vikali shambulio hilo dhidi ya walinda amani.

“Kwa miezi kadhaa sasa, tumekuwa tukiendesha operesheni za kiusalama kwenye eneo hili la Mali, na lengo kuu ni kusaidia kupunguza ghasia dhidi ya raia, kurejesha utulivu kwenye maeneo ambako kumeripotiwa mvutano bainaya jamii na pia kupunguza vitisho vya vilipuzi vya kutengenezwa kwenye maeneo kadhaa kama ilivyo kwenye eneo la Douentza,” amesema Bwana Annadif kwenye taarifa hiyo.

Mkuu huyo wa MINUSMA amesema operesheni hizo zimekuwa ‘mwiba’ kwa maadui wa amani lakini “tumeazimia kuwa sambamba na wananchi wa Mali kwa ajili ya Mali.”

Halikadhalika amehakikisha kuwa hatua zote zinachukuliwa kuhakikisha kuwa walinda amani waliojeruhiwa wanapta matibabu ya kina nay a haraka huku akiwatakia ahueni ya haraka.