Ukuzaji wa Kiswahili uwe na bajeti maalum

22 Januari 2021

Nchini Tanzania wiki hii kumefanyika tamasha la lugha ya Kiswahili lililoenda sambamba na utoaji wa tuzo za umahiri wa lugha hiyo ambapo Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ilikuwa mshindi katika kipengele cha ukuzaji wa msamiati.

Pamoja na utoaji wa tuzo hizo, waandaji wa tamasha hilo, Baraza la Kiswahili la Taifa Tanzania, BAKITA, na Baraza la Kiswahili Zanzibar, BAKIZA walitoa fursa kwa mijadala ya kujadili mbinu za kukuza na kuendeleza lugha hiyo adhimu.

Tamasha lilifanyika kwa siku mbili huko Dodoma, mji mkuu wa Tanzania na kufunguliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye yeye pamoja na mambo mengine ametaka kuwepo na bajeti maalum ya kukuza lugha ya Kiswahili.

Bi. Samia amesema mara nyingi hakuna bajeti maalum la kukuza lugha hiyo na inapotengwa fedha ni uamuzi tu wa mkurugenzi wa idara husika hivyo “wito wang una wito wa wataalamu wengi kuwepo na sera maalum ya Kiswahili kwa kuwa sera itazingatia yote hayo.”

 

Lugha ya Kiswahili inasambaa lakini ina fursa na soko gani? Mhadhiri Mwandamizi wa Tafsiri na Taaluma za Kiswahili Dk.Hadija Jilala kutoka Tanzania amesema, “kwa upande wa lugha ya kiswahili, fursa yake ni pana sana kwa maana kuna fursa nyingi mtu anaweza kujiajiri kama mtu binafsi au taasisi zinaweza kupata mapato. Tuna fursa kama uandishi na uchapishaji, uhariri, tafsiri na ukalimani, kufundisha lugha ya kiswahili kwa wageni na pia fursa ya kufundisha namna ya kufundisha lugha kwa wageni.”

Akagusia pia changamoto zinazokabili waandishi wa vitabu akawasihi kutumia ukuaji wa teknolojia kama nyanja ya kukuza Kiswahili akisema ni suala ambalo ni gumu kwa kuwa watanzania hawana utamaduni wa kusoma, kwa hiyo inakuwa ni kazi sana kumpatia mapato mwandishi anapoandika. Mchakato wa uchapishaji unaanzia kwa mwandishi mwenyewe kuwa na wazo, kuandika anatumia muda wake mwingi kukaa na kuandika na kurekebisha rasimu mbali mbali za muswada wake anaoandika mpaka umfikie mchapishaji.

“Utoke kwa mchapishaji ndio uende kwa mlaji. Hata kwa wanafunzi wetu wanachukua kitabu wanatoa nakala na mapato kwa mwandishi yanakuwa hayapatikani. Waandishi wengi wa vitabu bado hawajatumia fursa ya teknolojia na kuweka vitabu vyao. Watu tunatakiwa tuitumie." Amesema Dkt. Jilala. 

Wanawake nao wana fursa katika uandishi wa vitabu ambapo Dkt. Jilala amewataka watumie vyema vipaji vyao badala ya kujificha akiwataka kuwa tayari kujifunza kwa wengine kukuza uwezo wao.

Dkt. Jilala amesema mwamko bado si mkubwa sana na kama ambavyo hakuna utamaduni wa kusoma vivyo hivyo utamaduni wa kuandika ni mdogo. Amesema wengi wanaoandika vitabu mara nyingi wako kwenye taasisi za elimu. “Bado tuna wanawake wachache sana wanaoandika vitabu nchini, wanahitaji kupatiwa uhamasishaji. Kwa sababu mwanamke anarekebisha jamii, na mwanamke ndio jukumu lake kama mama anajitajika kurithisha amali  za jamii kwa jamii.”

Kiswahili ni bidhaa ambayo hata wageni wanaihitaji na ndio maana Tunku Kiobya mmliki wa kituo cha kufundisha Kiswahili kwa  wageni Iringa (LILINGA SWAHILI SCHOOL) anafunguka akisema kuwa “tunao wateja wengi wanakuja kwetu na wanafanya vizuri kule wanakofanya kazi na wanawasiliana vizuri na watanzania. Marekani, Uingereza na Ujerumani wanaongoza kwa kuja kupata mafunzo. Wenzetu kwenye mashirika yao sera ni lazima wajifunze lugha na utamaduni wa Tanzania."
 
Aldin Mutembei ambaye ni Profesa Mshiriki Chuo Kikuu cha Dar es salaam na anasema watu wenye ulemavu wasisahaulike katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili akisema kuwa “ni kwa vipi lugha hii inawajali pia watu wenye ulemavu. Kila mara tunapokuwa na mkutano tunahakikisha kuna wakalimani wa lugha ya alama. Hata katika machapisho tunasisitiza umuhimu wa kujali watu wenye ulemavu wa kutoona au wenye uoni hafifu.”

Octavian Malaba ni mkalimani wa lugha ya alama naye akapaza sauti juu ya mtazamo wa jamii kwao na wito wao kwa BAKITA katika kukuza lugha ya alama.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter