Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lugha ya kiswahili ni fursa Watanzania ichangamkieni : Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia kwa njia ya video washiriki wa maadhimisho ya pili ya siku ya Kiswahili Duniani kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani tarehe 7 Julai 2023.
UN News
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia kwa njia ya video washiriki wa maadhimisho ya pili ya siku ya Kiswahili Duniani kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani tarehe 7 Julai 2023.

Lugha ya kiswahili ni fursa Watanzania ichangamkieni : Samia Suluhu Hassan

Utamaduni na Elimu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Kiswahili lkuwa lugha ya kimataifa ni fursa nzuri na muhimu ambayo watu wa taifa lake wanapaswa kuikumbatia kwa mikono miwili.

Kupitia ujumbe wake wa video kwenye maadhimisho ya siku ya lugha ya Kiswahili duniani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Rais huyo amesema “Maadhimisho haya hayakuja ghafla bali yametokana na mchango uliofanywa na wanazuoni, wanaharakati, na watafiti mbalimbali ambao kwa moyo wao wa dhati waliandaa andiko, walijenga hoja na kuonyesha ushahidi kwamba , Kiswahili sasa si lugha tu ya Tanzania, Afrika Mashariki na nchi za maziwa makuu bali ni lugha ya Afrika na iliyoenea duniani kote.”

Amesema hoja zao ndizo zilizolifanya shirika la UNESCO kuitangaza siku maalum ya kuienzi lugha hii.

Maudhui ya mwaka huu yanaainisha kuibuliwa kwa uwezo wa Kiswahili katika zama hizo za kidijitali ambapo Rais samia amesema hilo litaongeza fursa zaidi kwa wananchi wa taifa lake , fursa ambazo anataka kila mtu azikumbatie huku akisistiza kwamba jukumu la kukiendeleza na kukiza Kiswahili liko mikononi mwao.

“Niwahakikishie kuwa Tanzania imeweka mikakati ya kuwahamasisha watanzania wenye weledi katika lugha ya Kiswahili kuchangamkia fursa zitokanazo na kukua kwa lugha kama vile ukalimani, utafsiri, uhariri , uhandishi wa habari, uandishi wa vitabu, utangazaji , na ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni na hata utungaji na uimbaji wa nyimbo na muziki.”

Amesisitiza kuwa Tanzania kama kitovu cha lugha hiyo haina budi kukipa nguvu na kuongeza matumizi yake katika nyanja za kiuchumi , kidiplomasia sayansi na teknolojia.

Amehitimisha ujumbe wake kwa wito kwa wakuu w anchi na serikali “Kuhamasisha kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili katika nchi zao kwa kuwa matumizi ya lugha hii ni mapana zaidi na yenye tija.”