Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano maalumu na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuhusu Kiswahili kutambulika kimataifa 

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia mjadala wa viongozi kuhusu mshikamano kwenye mkutano wa COP26 huko Glasgow, Scotland
UN WebTV Video
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia mjadala wa viongozi kuhusu mshikamano kwenye mkutano wa COP26 huko Glasgow, Scotland

Mahojiano maalumu na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuhusu Kiswahili kutambulika kimataifa 

Utamaduni na Elimu

Kufuatia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO mwishoni mwa mwaka jana 23 mwezi Novemba mwaka jana 2021 kuitambua lugha ya Kiswahili kuwa moja ya lugha za kimataifa na kuitengea siku yake maalumu Julai 7 kila mwaka, kwa mara ya kwanza mwezi huu, kote duniani siku hii itaadhimishwa kwa namna mbalimbali.  

Miezi kadhaa kabla ya maamuzi hayo ya kihistoria, tayari Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikuwa ameieleza Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kupitia mahojiano yaliyofanyika mwezi Septemba jijini New York, Marekani kuwa alikuwa amekusudia kuhutubia mjadala mkuu wa wazi wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa akionesha wazi kuwa ingawa hilo halikutokea lakini nia ya kufanya hivyo katika mikutano ijayo anayo bado. 

Rais Samia Suluhu Hassan akihojiwa na Anold Kayanda wa UN News Kiswahili, jijini New York Marekani baada ya UNGA76. (23 Septemba 2021)
Ikulu-Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan akihojiwa na Anold Kayanda wa UN News Kiswahili, jijini New York Marekani baada ya UNGA76. (23 Septemba 2021)

Sasa zikiwa zimesalia siku zinazohesabika kuelekea Siku ya Kiswahili Duniani, Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, imefanya tena mahojiano maalumu na Rais Samia ili kupata maoni yake kuhusu hatua hizo za lugha ya Kiswahili kuendelea kukita mizizi na kushamiri ulimwenguni. 

UNESCO kuitambua kimataifa lugha ya Kiswahili kuna tija gani kwa watu wa Afrika na Tanzania kwa ujumla? 

“Ina tija kubwa na labda niseme kila safari huanza na tija za wali. Kwa hiyo kutambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa ina maana kwamba mataifa sasa yanakwenda kukitambua Kiswahili. Kwa sababu wao kule wataadhimisha, sisi tutaadhimisha zinazozungumza Kiswahili wataadhimisha. Ni imani yangu nchi kama Oman pia wataadhimisha kwa sababu nusu ya watu kule wanazungumza Kiswahili. Kwa hiyo, huo ni mwanzo wa hatua. Lakini hii hatua inatupeleka wapi? Inatupeleka sasa, Kiswahili kwenda kutumika kwenye nyanja mbalimbali katika majukwaa ya kimataifa. Na ndio maana nikasema kila safari huanza na hatua zaa wali. Kwa hivyo hatua zaa wali ni kutambulika. Kwa hivyo wata watakavyosoma, watakavyokitumia, kitakwenda kutumika kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa.” 

Maadhimisho haya ya kwanza kabisa ya siku ya lugha ya Kiswahili yatakayofanyika Julai 7 yanamaanisha nini kwake na taifa lake la Tanzania linaloaminika kuwa chimbuko la lugha hii adhimu ya Kiswahili? 

“Maadhimisho haya yana maana kubwa kwetu kwamba sisi wenye chimbuko la lugha tumetambuliwa kimataifa na kwamba shirika la Umoja wa Mataifa limeweka siku maalumu ya kuadhimisha Kiswahili tukitambua kuwa ni lugha ya kwanza ya kiafrika kutambulika katika ngazi ya Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo kwa sisi kwanza ni heshima kubwa kwa taifa letu, lakini pia ni kunyanyua hadhi ya Tanzania, hadhi ya Afrika Mashariki, hadhi ya maeneo yale ambayo Kiswahili kinasemwa, na kwamba sasa Kiswahili kitasemwa kwa upana zaidi. Tukielewa kwamba hata nje Ulaya na Marekani, watu wanasoma sana Kiswahili. Sasa kuwekwa siku hii maalumu ya kimataifa ya Kiswahili, itafanya watu wakisome sana Kiswahili. Kwa hiyo kwetu sisi siku hii ina maana kubwa kwetu. Na kama mnavyoona tumejipanga vizuri kuiadhimisha siku hii ya Kiswahili.” 

Siku ya lugha ya Kiswahili duniani
UN
Siku ya lugha ya Kiswahili duniani

Pamoja na Kiswahili kutambuliwa na UNESCO, bado lugha hii haijawa lugha rasmi katika Umoja wa Mataifa, kuna jitihada gani zinafanyika kuifikisha huko ili iungane na lugha nyingine sita rasmi?  

“Hata hizo lugha zinazotambulika sasa hivi ndani ya Umoja wa Mataifa hazikuanza kuingia tu kiharaka hivyo. Lazima kazi ilifanya mpaka kufikia huko na ukaonekana umuhimu wa hizo lugha kuingizwa huko. Sasa kwa sababu Kiswahili kimetambulika kimataifa, kitazunumzwa na mataifa mengi, watu mataifa mengi watajifunza, ndio lugha pekee ya kiafrika ambayo imetambulika, ni imani yetu kwamba si muda mrefu sana, kiswahili kitazungumzwa ndani ya Umoja wa Mataifa. Kwa sababu kwanza, jitihada zinazofanywa, Kiswahili ni lugha rasmi ndani ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Lakini Kiswahili kimeshakubalika SADC na kwenyewe kinatambulika. Na kwenye Umoja wa Afrika, AU, jitihada zinafanywa imeshatambulika, kuna mambo ya kumalizia ambayo Tanzania tumebeba kama sisi wenye lugha tumebeba kuyamalizia ili Umoja wa Afrika nao uzungumze Kiswahili kama Lugha rasmi. Kwa hivyo tukienda kwenye hizo, Afrika Mashariki, kusini mwa ukanda wa Afrika, SADC, na Umoja wenyewe wa Afrika, basi Kiswahili kinagonga hodi pia kwenye Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo jitihada tunazofanya, tumeshafanya jitihada kwenda kwenye majukwaa matatu makubwa, na hilo jukwaa la nne tuna hakika Kiswahili kitafika na kitazungumzwa huko.”  

Rais Samia Suluhu Hassan ana ujumbe gani kuelekea siku yenyewe ya Kiswahili Duniani Julai, 7? 

“Mimi ujumbe wangu ni kwanba tukikuze Kiswahili. Kwa sababu ukija kwenye Afrika Mashariki, ambako tumeshakubaliana kuwa Kiswahili ni moja ya Lugha za kufanyia kazi katika Jumuiya yetu, Kiswahili kinazungumzwa karibu katika nchi zote isipokuwa Sudan Kusini.Lakini ukienda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wana Kiswahili cha aina yao, Kenya wana Kiswahili chao, wanyarwanda wanaongea Kiswahili, warundi wanaongea Kiswahili sana, Uganda wanaongea Kiswahili, na sisi ndio wenyewe hapa. Kwa hiyo ndani ya Afrika Mashariki Kiswahili ni lugha kubwa inayounganisha watu wengi wa Afrika Mashariki. Lakini jingine ni kwamba lugha hii, hata ukienda Afrika Kusini kwa mfano, nchi nyingi hasa zile tulizosaidiana nazo kwenye ukombozi, nyingi zile zinazungumza Kiswahili. Na bahati nzuri kwa wale wenzetu wa kusini, lugha ya Kishona kinafanana kabisa na Kiswahili. Mshona akiongea unaweza ukamuelewa vizuri, na mshona ukiongea anakuelewa vizuri. Maneno mengi ni yale yale yanafanana. Kwa hivyo utaona ilivyosambaa. Lakini, lugha hii, inakwenda kuunganisha sekta kubwa sana ya vijana na wafanyabiashara ndogondogo.” 

Kukubalika Kiswahili kimataifa kutabadili mwelekeo wa lugha ya kufundishia Tanzania? 

“Hili limeshajadiliwa sana Tanzania, wananchi wamelijadili, bungeni wamelijadili. Wizara ya elimu sasa iko kwenye hatua za kuhoji wananchi mabadiliko ya mitaala ya kufundisha wanafunzi wetu Tanzania. Kwa hivyo inawezekana kwamba hili la lugha nalo likawa moja ya vipengele vitakavyojadiliwa. Lakini kwa Kiswahili kutambulika kimataifa, hiyo inagonga kengele kwetu kwamba, hata watoto wetu hapa tunaweza tukawafundisha kwa Kiswahili kwa sababu inakwenda kuwa lugha ya kimataifa. Lakini pia niseme kuna tafiti mbalimbali ulimwenguni na hapa ndani, zinazoonesha kwamba ukimfundisha mtoto kwa lugha anayoielewa, anaelewa vizuri zaidi, anafaulu vizuri kuliko ukimfundisha kwa lugha ya kigeni ambayo anaisoma tu shule na muda mwingi anatumia lugha nyingine. Sasa na sisi jitihada tunazozifanya humu ndani, Baraza letu la Kiswahili la Taifa (BAKITA), linatoa tafsiri ya maneno mbalimbali kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili. Wanajitahidi kufanya hivyo ili watoto waweze kujua na kuelewa kwa haraka. Lakini pia sasa hivi tunayo haya mambo ya kisayansi ya kompyuta, kwa hivyo kwenye Baraza kuna timu maalumu inayotafsi mambo haya ya kisayansi katika lugha ya Kiswahili. Lakin jingine, mahakama zetu sasa hivi tulisema hukumu zitoke kwa Kiswahili kwa hiyo mahakama zimefanya jitihada, ngazi fulani za mahakama tayari hukumu zimeanza kutoka za Kiswahili. Kwa hiyo hiyo yote inatupeleka kwamba hata shuleni watoto wetu tukawafundishe kwa lugha wanayoifahamu, lugha ambayo wataitumia katika maeneo kadhaa, lugha ambayo tayari imeshatafsiriwa, kisanyansi imetafsiriwa, haya mambo ya sasa hivi ya ICT inatafsrirwa. Kwa hiyo nadhani tuko kwenye hatua nzuri. Mpaka tulipofika sasa hivi siwezi kukwambia tutafundisha hatufundishi lakini kwa jinsi Kiswahili kinavyokwenda, nadhani, tutaelekea mwelekeo huo.”  

Kamusi ya Kiswahili toleo la 3 ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dr.phillip Mpango kwenye Kongamano la dunia la Kiswahili
UN/ Stella Vuzo
Kamusi ya Kiswahili toleo la 3 ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dr.phillip Mpango kwenye Kongamano la dunia la Kiswahili