Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatiwa hofu na wanaokimbia ghasia CAR

Zaidi ya watu 12,000 wameripotiwa kukimbia Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na kuingia nchini DR Congo.
© UNHCR/Ghislaine Nentobo
Zaidi ya watu 12,000 wameripotiwa kukimbia Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na kuingia nchini DR Congo.

UNHCR yatiwa hofu na wanaokimbia ghasia CAR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema lina hofu kubwa ya kwamba ghasia na ukosefu wa usalama vitokanavyo na uchaguzi mkuu wa tarehe 27 mwezi uliopita nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, vimesababisha zaidi ya watu 30,000 kukimbilia nchi jirani za Cameroon, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Jamhuri ya Congo.
 

 Msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswisi Boris Cheshirkov amewaeleza waandishi wa habari kuwa kando ya hao waliokimbilia nchi jirani, makumi kadhaa wamesalia wakimbizi ndani ya nchi yao.

UNHCR inasema kuwa mashambulizi ya tarehe 2 na 3 mwezi huu wa Januari huko Damara na Bangassou yamelazimisha maelfu ya raia kuvuka mto Ubangui na kuingia majimbo ya Bas Uele na Ubangi Kaskazini nchini DRC. Hali ni mbaya zaidi kwa watu 15,000 waliokimbilia kijiji cha Ndu nchini DRC kwa kuwa kijiji hicho kina wakazi 3,500 na kimezidiwa uwezo wa huduma kwa wakimbizi na wenyeji wao,

Hata hivyo UNHCR imeimarisha uwepo wake kwenye mto Ubangi ili kukidhi mahitaji ya wanaowasili na kuandaa kazi ya kuwasajili na makazi ya muda ambako watahamishiwa kwa ajili ya usalama zaidi.

Huko Cameroon nako waliokimbilia ni 4.434 na wengi wao waok kwenye eneo la mpakani la Garoua-Boulai ilhali wengine 2.196 wamewasili Chad na takribani 70 wameingia Jamhuri ya Congo.
Ingawa baadhi ya wakimbizi wa ndani nchini CAR wameripotiwa kurejea katika makazi yao, UNHCR ina hofu juu ya ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu na imetoa wito kwa mamlaka katika nchi jirani ziendelee kuwapatia hifadhi na kusadia mamlaka za mitaa kusajili wakimbizi wapya.

Kwa mujibu wa Bwana Cheshirkov, wakimbizi wengi wanaishi na jamii wenyeji au katika makazi ya kuhamahama. “Hivi sasa wanahitaji maji, makazi na huduma za kutosha za afya na za kujisafi ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 na magonjwa mengine”.

UNHCR inasema inashirikiana na mamlaka katika nchi husika pamoja na wadau kuwapatia wakimbizi hao ulinzi, mathalani nchini Cameroon kuna eneo maalum huko Gado ambako wanaowasili wanasajiliwa.
Halikadhalika nchini Chad, shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, linatoa mgao wa vyakula kwa wakimbizi wapya huku UNHCR ikitoa huduma za afya kupitia kliniki iliyoko kwenye gari.

Kufuatia ghasia hizo mpya nchini CAR, operesheni ya wananchi wa CAR waliokuwa wanarejea nyumbani kwa hiari kutoka Cameroon na DRC tangu mwezi Novemba mwaka 2020 sasa imesitishwa kwa muda.

TAGS: UNHCR, WFP, CAR