Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je unawezaje kuanza upya maisha ukiwa umepoteza kila kitu:Mkimbizi Fidel

Wakimbizi nchini DRC.
OCHA/Otto Bakano
Wakimbizi nchini DRC.

Je unawezaje kuanza upya maisha ukiwa umepoteza kila kitu:Mkimbizi Fidel

Wahamiaji na Wakimbizi

Kutana na mkimbizi Fidel kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR ambaye hivi sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. Fidel alipoteza kila kitu ikiwa ni pamoja na mwanaye wa kiume machafuko yaliposhika kasi CAR na ikamlazimu kufungasha virago na kukimbia, sasa anajaribu kujenga upya maisha yake ukimbizini.

Katika kambi ya wakimbizi Mashariki mwa DRC, Fidel anajaribu kufanya kila awezalo kufungua ukurasa mpya wa maisha yake ukimbizini.  

Yeye na familia yake walifunga virago mwezi Januari mwaka huu na kukimbia mapigano yaliyopamba moto CAR wakielekera nchi jirani kusaka usalama na kabla ya kifika DRC  Fidel alipoteza mwanaye “Niliwauliza kaka zangu mwanangu yuko wapi? Wakasema hawajamuona, mtoto alitumbukia kwenye maji, alizama alikuwa anaitwa Eric”. 

Fidel anasema asilani hatosahau mkasa huo mkubwa. Hadi sasa kwa mujimu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR katika muda wa miezi minne tangu Januari mwaka huu limeshaorodhesha wakimbizi 52,000 kutoka CAR ambao wanapata hifadhi DRC. 

Wengi wa wakimbizi hawa walikuwa wakiishi katika mazingira magumu mpakani na sasa shirika hilo linazihamishia familia za wakimbizi hawa kwenye maeneo salama ambako linawapa msaada pamoja na jamii zinazowahifadhi. 

Katika makazi hayo mapya UNHCR inasema inahitaji fedha zaidi ili kukidhi mahitaji yao. Kwa wakimbizi hao kama Fidel na familia yake anasema wanapata matumaini kwani wako salama na wana imani watoto wao wataweza kupata fursa ya kwenda shule na kuishi bila hofu wakijaribu kujijenga upya maisha hadi pale itakapokuwa salama kurejea nyumbani kwani“Siku nilipokimbia nilipoteza kila kitu change, baiskeli na hata fedha nilizokuwa nazo. Kila kitu kilipotea. Watoto wangu walikuwa wakienda shule. Endapo watasoma huo ndio utakuwa mustakbali wangu.”