Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu waendelea kufungasha virago CAR na kuingia Cameroon kusaka usalama:UNHCR

Picha hii kutoka maktaba ikionesha raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) wakivuka mpaka kwa miguu na kuingia Chad.
© IOM/ Craig Murphy
Picha hii kutoka maktaba ikionesha raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) wakivuka mpaka kwa miguu na kuingia Chad.

Maelfu waendelea kufungasha virago CAR na kuingia Cameroon kusaka usalama:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Watu zaidi ya 5,000 wamefungasha virago siku za karibuni wakikimbia mashambulizi ya waasi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR hasa kwenye mji wa Magharibi wa Bouar na kuingia nchi jirani ya Cameroon kusaka usalama, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Katika makazi ya wakimbizi ya Garoua Boulai nchini Cameroon maelfu ya watu wamewasili hivi karibuni kutoka CAR wengi wakiwa wanawake na watoto wamekusanyika wanasubiri kusajiliwa na shirika la wakimbizi UNHCR.  

Wamekimbia vijiji vyao Bouar kwa kuhofia usalama wao baada ya uvumi kwamba waasi wanakaribia mji mkuu Bangui.  Miongoni mwao ni mkimbizi Josephine Loumarou, "Siku si nyingi tulibaini kwamba waasi wako kilometa 30  tu kutoka Bouar. Walikuja kuvamia Bouar, na kushambulia kwa kutumia silaha kubwakubwa.” 

Kwa mujibu wa UNHCR kuna kila dalili kwamba makundi hayo yenye silaha yatashambulia katika sehemu mbalimbali za CAR na ingawa mipaka baina ya CAR, Cameroon na Chad imefungwa UNHCR inaendelea kuzisihi nchi hizo kuiacha wazi ili wanaokimbia kwendfa kusaka usalama waweze kunusuru maisha yao. Ihondou Melina mmoja wa wakimbizi hao anasema hakuwa na jinsi bali kuacha kila kitu ili yeye na mumewe waokoe maisha yao,“Kwa hakika tulipata pigo kubwa sana kwa kuwasili kwa waasi hao. Na hivyo ilitubidi mimi na mume wangu kuacha vyote na kukimbia , tukiamini kwamba huenda nasi tutapata amani.” 

Ingawa kwa sasa mjini Bouar hali imeanza kutulia lakini bado kuna uvumi kwamba kundi lenye silaha linapanga kushambulia kituo cha mpango wa MINUSCA cha walindamanani wa Umoja wa Mataifa nchini CAR na kambi ya vikosi vya serikali endapo mahakama ya katiba itathibitisha uchaguzi wa Rais Touadéra. 

Pamoja na UNHCR kuwasajili na kuwasaidia wakimbizi hawa sasa,  hatma yao haijulikani. 

Shirika hilo linajenga malazi ya dharura kwa familia 300 kwenye kambi ya karibu ya Gado Cameroon ambayo tayari inahifadhi wakimbizi 26,000 ambao hawawezi kurejea nyumbani sababu ya usalama.