Wakimbizi wa CAR warejea nyumbani wakitaka nchi yao sasa iwatunze

4 Disemba 2019

Kundi la nne la wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR waliokuwa wamekimbilia nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, limerejea nyumbani na kulakiwa na Kamishna Mkuu wa wakimbizi duniani, Filippo Grandi, huku wakiwa na matumaini ya maisha mapya.

Wakimbizi hawa wanaondokea eneo la zongo, wakivuka mto Oubangui, unaotenganisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Jamhuri ya Afrika ya  Kati, CAR.

Wanarejea nyumbani tangu wakimbie CAR miaka 6 iliyopita lakini sasa mkataba wa kurejea nyumbani kwa hiari uliotiwa saini kati ya serikali na UNHCR umewezesha kurejea kwao.

Wakimbizi hawa 200, ikiwa ni wanawake, wanaume na watoto hawakuficha hisia zao za kurejea nyumbani wakiimba, Asante DRC! Asante UNHCR! Jamhuri ya Afrika ya Kati! nchi yangu nzuri!..

Punde wanawasili bandari ya Bangui na miongoni mwao ni Marie Joseph Demba ambaye anasema kuwa, “matumaini  yangu ni kwamba nimerejea nchini mwangu. Sasa nataka nchi yangu initunze, tuko wengi hapa na kuna watoto, watu walio hatarini. Tunataka serikali itusaidie.”

Reno Mauwina ni mhandisi wa ujenzi mwenye umri wa miaka 42 ambaye alikimbia ghasia mjini Bangui mwaka 2013. Yeye ana familia ya watu 7 na watoto wake wawili walizaliwa ukimbizi na sasa baada ya kurejea anasema, “hofu ni kwamba kilichochochea ghasia bado kinaweza kutokea tena. Hatuna uwezo wa kukabiliana nacho tena. Tuna matumaini kuwa watoto wetu wamereja kwenye mazingira ya amani.”

Katika bandari ya Oubangui wanalakiwa na Kamishna Mkuu wa shirika la wakimbizi duninia, UNHCR, Filippo Grandi akiwa na Waziri wa masuala ya kibinadamu wa CAR.

Bwana Grandi anasema ingawa kuna changamoto za kukidhi mahitaji yao, ukweli ni kwamba kurejea kwao “ni dalili ya kuwa na imani na mustakabali wa amani na ni ishara ya ujasiri na imani kwenye amani. Tunapaswa kuendelea kujenga mifumo na mipango nchini kote hapa CAR baada ya machungu yote ili kila mtu anaweza kuchukua hatua hii ya kurejea nyumbani.”

Zaidi ya wakimbizi 1,400 wamesharejea CAR kutoka DRC tangu kuanza kwa zoezi la kuwarejesha nyumbani mwezi Desemba mwaka 2013. Wengine wengi pia wamerejea kutoka Cameroon na Jamhuri ya Congo.

Inakadiriwa kuwa wakimbizi 600,000 wa CAR wamesaka hifadhi nje ya nchi ilhali 650,00 ni wakimbizi wa ndani katika taifa hilo lenye jumla ya watu wasiozidi milioni 4.7.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud