Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la machafuko CAR linatia hofu kubwa: OCHA 

Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui
UN photo / Catianne Tijerina
Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui

Ongezeko la machafuko CAR linatia hofu kubwa: OCHA 

Amani na Usalama

Mapigano na mivutano iliyoshuhudiwa wiki iliyopita nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, ina athari kubwa kwa ulinzi wa raia nchini humo limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Bangui mratibu wa OCHA nchini humo Denise Brown ameelezea hofu yake kubwa kwa kuendelea kwa machafuko hayo katika sehemu mbalimbali za nchi hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii 27 Desemba. 

Amesema “Kutokuwepo kwa usalama na hofu ya mashambulizi tayari vimezusha taharuki kwa wanannchi na kusababisha watu zaidi ya 55,000 kufungasha virago na kuzikimbia nyumba zao hali ambayo inawaongezea hatari watu hao.” 

Ameongeza kuwa makundi yenye silaha pia yameongeza vitisho na mashambulizi dhidi ya wahudumu wa kibinadamu ambao wamejitoa kimasomaso kusaidia watu wa CAR. 

Taarifa yake inasema wiki iliyopita pekee kumeorodheshwa matukio zaidi ya 17 dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu na mali zao. 

Na zaidi ya hapo gari la kubeba wagonjwa na gari lingine kutoka kituo cha afya cha wilaya yalivamiwa na muhudumu mmoja wa afya kujeruhiwa. 

Denise Brown amesema “Hali hii imewafanya maelfu ya watu katika eneo la Magharibi na Kati mwa nchi hiyo kushindwa kupata msaada wa dharura hususan msaada wa huduma za afya.” 

Kwa mantiki hiyo Bi. Brown amesema “Ninalaani vikali vitendo hivi vya machafuko ambavyo vinaongeza madhila na athari kwa watu wa CAR na ninatoa wito kwa makundi yenye silaha kukomesha mara moja mashambulizi dhidi ya wahudumu wa kibinadamu na kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu na kulinda raia na miundombinu yao.” 

Hata hivyo kwa mujibu wa OCHA licha ya kutokuwepo na usalama na changamoto za fursa ya kuwafikia wenye mahitaji wadau wa misaada ya kibinadamu wameendelea kufikisha msaada wa kuokoa maisha katika sehemu mbalimbali nchini humo, kupeleka timu za dharura za huduma za afya na kusafirisha kwa njia ya anga lishe na dawa kwa wenye uhitaji mkubwa. 

“Wahudumu wa kibinadamu wanaendelea kusalia kwenye jamii licha ya machafuko ambayo lazima yakome.” Amesisitiza Bi. Brown. 

Mratibu huyo pia wa masuala ya kibinadamu ametoa wito kwa wahisani kuongeza ufadhili wa haraka kwa ajili ya kuchukua hatua za misada ya kibinadamu CAR ikiwemo huduma za usafiri wa anga za Umoja wa Mataifa . 

Pia amesema watu milioni 2.8 wanahitaji msaada na ulinzi na mahitaji ya kibinadamu mwaka 2021 yanahitaji dola milioni 444.7 kuweza kusaidia watu milioni 1.8.