Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

 Chondechonde vijana tuache itikadi kali, tukumbatie amani Sahel: Vieux Farka Touré.

Mwanamuziki kutoka Mali na mpiga gitaa Vieux Farka Touré
Andy Boyle
Mwanamuziki kutoka Mali na mpiga gitaa Vieux Farka Touré

 Chondechonde vijana tuache itikadi kali, tukumbatie amani Sahel: Vieux Farka Touré.

Amani na Usalama

 Mradi wa kuelimisha kuhusu ongezeko la machafuko , kutokuwepo usalama na watu kutawanywa kwenye eneo la Sahel umefanya kutungwa wimbo mahsusi na mtunzi kutoka Mali Vieux Farka Touré na kuimbwa na wanamuziki mbalimbali wa eneo hilo. 

Kwa ushirikiano na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA, wimbo wa bwana Touré kwa ajili ya Sahel unaainisha machafuko yaliyoghubika nchi nyingi za ukanda wa Sahel huku pia ukitanabaisha urityhi wa hazina ya muziki kwenye ukanda huo. 

Katika mahojiano maalum na UN News mwanamuziki huyo anayeheshimika sana  ameeelezea ni kwa jinsi gani ambavyo ana hofia kusafiri kwenda nchi nzima kufanya matamasha ya muziki kama alivyokuwa akifanya zamani. 

“Watu wa Mali hivi sasa wanalala jicho moja wazi” Amesema mwanamuziki huyo akiongelea uasi unaoongozwa na watu wenye itikadi kali ambao wanatumia fursa ya kutokuwepo kwa nafasi za maendeleo kwa vijana wa taifa hilo. 

Ameongeza kuwa “Vijana lazima waonyeshe ujasiri, uimafra na kupinga mgogoro huu. Amani na mshikamano ndio nyenzo. Endapo amani itajengwa sasa Watoto wetu kesho watashamiri. Muziki ni nyenzo bora ya kupitisha ujumbe na kuelimishana ni suala la muhimu sana, lina athari nzuri kwa kile kinachoendelea katika nchi zetu.” 

Dharura inayokuwa kwa kasi 

Mgogoro wa Sahel ni moja ya dharura inayokuwa kwa kasi zaidi duniani. Kwa mujibu wa OCHA mwaka huu karibu watu milioni 29 wanahitaji msaada wa kuokoa maisha na ulinzi , idadi ambayo ni watu milioni 5 zaidi yam waka jana. 

Wakati hali ya kibinadamu ikiendelea kuzorota kwa haraka , shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba hali mbaya ya watu inasababishwa na ongezeko la machafuko, kutokuwa na uhakika wa chakula, kuongezeka kwa dharura za mabadiliko ya tabianchi na janga la COVID-19

Matumaini ya OCHA ni kwamba wimbo kwa ajili ya Sahel utatoa matumaini japo kidogo kwa wote wanaohitaji msaada leo hii. 

“Wimbo huu unasherehekea mnepo, ukarimu, mshikamano na uimara ambao unaendelea kuonyeshwa na watu wa Sahel licha ya mgogoro unaowaghubika, pamoja na urithi wa utamaduni wao wa muziki” amesema Bounena Sidi Mouhamed, naibu mkuu wa OCHA kanda ya Afrika Magharibi na Kati. 

Amani na usalama 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa akisisitiza hofu yake juu ya Ukanda wa Sahel barani Afrika ambako hali ya usalama inazorota na machafuko yanayoendelea yanazidisha hali iliyokuwa mbaya ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi. 

Amesema na hali hiyo inaongezwa madhila kutokana na kuendelea kwa janga la Corona au COVID-19 na dharura ya mabadiliko ya tabianchi.