Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan imehimizwa kuimarisha ulinzi, kurejesha amani kufuatia machafuko Darfur Magharibi

Walinda amani wa UNAMID wakipiga doria mnamo Juni 2018 Masteri, Darfur Maghribi kama sehemu ya wajibu wake ujumbe huo kulinda raia eneo la Darfur, Sudan.
UN Photo/Surendra Bahadur Ter
Walinda amani wa UNAMID wakipiga doria mnamo Juni 2018 Masteri, Darfur Maghribi kama sehemu ya wajibu wake ujumbe huo kulinda raia eneo la Darfur, Sudan.

Sudan imehimizwa kuimarisha ulinzi, kurejesha amani kufuatia machafuko Darfur Magharibi

Amani na Usalama

Mamlaka nchni Sudan imehimizwa kurejesha amani na utulivu wakati huu ambapo kunashuhudiwa machafuko ya kikabila katika jimbo la Darfur magharibi ambayo yalizuka Jumapili iliyopita na kusababisha vifo vya watu 65, majeruhi 54 na maelfu ya watu kutawanywa.

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani jimboni Darfur, UNAMID umetoa ombi hilo kupitia tarifa yake iliyotolewa leo Ijumaa, huku ukielezea wasiwasi wake kuhusu hali inayoshuhudiwa.

Kwa mujibu wa wahudhumu wa kibinadamu, vijiji viliteketezwa na kambi za wakimbizi wa ndani kushambuliwa.

Taarifa hiyo imeunukuu ujumbe huo ukisema, “UNAMID inalaani ukatili uanotekelezwa na inahimiza umuhimu wa kutatua migawanyiko yoyote kwa njia ya amani, na inatoa wito kwa wadau kujizuia kutumia nguvu kupita kiasi, hususan dhidi ya raia ikiwemo wanawake na watoto.”

Inakadiriwa kwamba watu 30,000 walilazimika kukimbia makwao na kusaka hifadhi karibu na ndani ya mji mkuu wa El Geneina imesema ofisi ya Umoja 

wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA.

Washikadau wanafanya juhudi za kuchunguza idadi ya watu waliotawanywa walio na mahitaji zaidi ikiwemo makazi, chakula, maji na huduma za afya.

UNAMID pia imesafirisha wafanyakazi 32 wa misaada ya kibinadamu hadi Zalingei, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kati kufuatia wasiwasi kuhusu usalama wao.

Na kusema “wakati tukizingatia juhudi za serikali katika kukabiliana na hali, tunatoa wito kwa mamlaka kuongeza nguvu zaidi katika kuweka mazingira bora na kurejesha amani na utulivu ndani na karibu na jamii El Geneina kwa ajili ya kuhakikisha mwendelezo wa utoaji wa misaada kwa jamii walio na mahitaji zaidi.