Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilimwambia mume wangu, tangulia na wa kiume, mimi nakuja na wa kike, tukikamatwa basi-Mkimbizi wa Ethiopia 

Wengi wa wakimbizi wanaokimbia eneo la Tigray walioko Um Raquba ni wanawake na watoto.
© UNFPA Sudan/Sufian Abdul-Mout
Wengi wa wakimbizi wanaokimbia eneo la Tigray walioko Um Raquba ni wanawake na watoto.

Nilimwambia mume wangu, tangulia na wa kiume, mimi nakuja na wa kike, tukikamatwa basi-Mkimbizi wa Ethiopia 

Wahamiaji na Wakimbizi

Mzozo wa Ethiopia ukiendelea, familia moja iliyotenganishwa walipokimbia eneo la Tigray la Ethiopia ina bahati ya kuungana tena nchini Sudan, lakini wasiwasi juu ya maisha yao ya baadaye ni mzito.

Hapa ni Hamdayet, Sudan. Wakimbizi wako katika uhitaji wa haraka wa msaada wakati  mashirika ya misaada ya kibinadamu yanajitahidi kukidhi mahitaji yanayoongezeka lakini zaidi ya yote, wakimbizi wanataka kuwa salama kurudi nyumbani na kuendelea na maisha yao.  

Tsiga na familia yake walifurahia maisha ya utulivu, ya kupendeza, wakilima ardhi yao katika mkoa wa Tigray wa Ethiopia, lakini wakati mzozo ulipozuka, alijua kuwa haikuwa salama tena kukaa katika shamba lao… 

Tsinga anasema, aliiambia familia yake wanapaswa kuondoka. Alimwambia mume wake kuwa aende na mtoto wao wa kiume na kisha yeye atafuata na binti yao. Kama huku nyuma atakamatwa, ni sawa tu. Mungu akipenda, watakutana. 

Mumewe na wanaume wengine katika kijiji chao walishikiliwa na watu wenye silaha kwa siku saba kisha wakaachiliwa, lakini hali hiyo iliwaacha na hisia mbaya. 

Familia hiyo ilikimbia kwa njia tofauti kuelekea Sudan, ikijua hawawezi kuonana tena. Kwa bahati nzuri, wameungana tena hapa Hamdayet katika kituo cha mapokezi chenye maelfu ya wakimbizi kutoka Ethiopia wanaokimbilia Sudan. Ingawa wako salama, wanajitahidi kuzoea hali ya hapa. 

"Hatuna mipango ya siku zijazo. Kila kitu tulichofanyia kazi sasa hakina faida. Tuko hapa tu tunalala chini bila hata kubadili nguo.” Anasema mwanamke huyu akilengwalengwa na chozi. 

Tsiga ana wasiwasi juu ya siku zijazo za familia yake na anahofia wamepoteza vitu vingi sana na anasema tangu mgogoro huu ulipoanza, hawajalala. Walikuwa na matumaini. Aliwasomesha watoto wake ili wawe na maisha bora. Alikuwa anasubiri mwanae wa kiume ahitimu Chuo Kikuu. 

Takribani Waethiopia 50,000 wamekimbilia Sudan, kufuatia mzozo huko Tigray. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, pamoja na maafisa wa Sudan, wamehamisha wakimbizi 12,000 kutoka Hamdayet na mpaka wa Abderafi hadi kambi ya Um Rakuba, iliyoko umbali wa kilomita 70 kutoka mpaka wa Ethiopia. 

Lakini mahitaji ni makubwa na mashirika ya kibinadamu yanajitahidi kusaidia kila mtu. Wakimbizi wengi katika kambi hiyo na wale wanaovuka kuingia Sudan ni wanawake na watoto. Wanahitaji chakula, malazi, maji safi, huduma za kujisafi na za afya. Pia kuna wasiwasi wa milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na maji.