Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi kutoka Tigray Ethiopia waendelea kumiminika Sudan:UNHCR 

Mzozo eneo la Tigray nchini Ethiopia umesababisha watu kukimbilia Hamdayet Sudan
© UNHCR/Hazim Elhag
Mzozo eneo la Tigray nchini Ethiopia umesababisha watu kukimbilia Hamdayet Sudan

Wakimbizi kutoka Tigray Ethiopia waendelea kumiminika Sudan:UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema mgogoro unaoendelea katika jimbo la Tigray Kaskazini mwa Ethiopia unazidi kuwa mbaya na kuwalazimisha maelfu ya watu kufungasha virago na kukimbilia nchi jirani ya Sudan nusu yao wakiwa ni watoto  hadi kufikia leo raia 27,000 wamewasili Sudan katika maeneo mbalimbali.

Katika eneo la milima la Hamdayet Sudan kwenye mpaka na Ethiopia mamia ya watu wakitembea kwa miguu kwenda kusaka usalama Sudan , wazee kwa vijana, wanaume kwa wanawake na pia watoto wakimbia machafuko yanayoendelea baina ya serikali na vikosi vya jimbo la Tigray. 

Baada ya kutembea kwa miguu kwa muda mrefu na kufika katika mto Hamdayet inabidi waingie katika mtumbwi kuvuka hadi  upande wa pili wa mji huo ambako  wanapokelewa na wenyeji wa mji huo.

Kwa mujibu wa UNHCR tangu kuzuka kwa machafuko mwanzoni mwa mwezi huu wa Novemba zaidi ya watu 15,000 wamewasili Sudan ambako mashirika ya misaada yanajitahidi kuwasaidia likiwemo shirika la UNHCR. Jens Hesemann mwakilishi msaidizi wa UNHCR amefika katika eneo hilo la mapokezi na anasema,“Hali ni mbaya sana, hivi sasa kuna takribani watu 15,000 hapa ambao wamekimbia na kuwasili katika siku tano zilizopita. Tumeanza kuwapa msaada, UNHCR, WFP, chama cha msalaba mwekundu cha Sudan, Muslim Aid na wadau wengine. Na unaweza kuona kuaanza kutolewa kwa baadhi ya misaada lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya.” 

Ameongeza kuwa idadi ya watu inatarajiwa kuongezeka hasa ukizingatia kwamnba watu zaidi ya 4,000 wanavuka mpaka kwa siku , lakini watu wa Hamdayet wamewakirimu wakimbizi hawa,“Hapa ni karibu sana na mpakani , huu ni mji wa Hamdayet na jamii hapa wamekuwa wakarimu wamekuwa wakitoa msaada kwa wakimbizi, wamewapa mahema, chakula na vifaa vingine. Hivyo tunaishukuru sana jamii ambayo imeubeba mzigo huu.” 

UNHCR inasema kituo cha mapokezi cha Hamdayet kina uwezo wa kuhifadhi wakimbizi 300 lakini sasa kimeshazidiwa uwezo kikiwa na wakimbizi 6,000, huku huduma za usafi kama vyoo ni haba na kuleta hofu ya magonjwa.