Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanaokimbia Tigray Ethiopia kuingia Sudan sasa imezidi 40,000: UNHCR 

Mkimbizi msichana kutoka Ethiopia akipokea godoro katika makazi ya muda Hamdayet Sudan.
© UNHCR/Olivier Jobard
Mkimbizi msichana kutoka Ethiopia akipokea godoro katika makazi ya muda Hamdayet Sudan.

Idadi ya wanaokimbia Tigray Ethiopia kuingia Sudan sasa imezidi 40,000: UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati idadi ya watu wanaokimbia jimbo la Tigray nchini Ethiopia kuingia mashariki mwa Sudan sasa imezidi 40,000, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linafanya jitihada kupata msaada wa kutosha unaohitajika kwa watu hao walio katika uhitaji mkubwa. 

Mgogoro unaozidi kuongezeka kaskazini mwa Ethiopia ambapo mapigano yanayoendelea kati ya serikali ya shirikisho la Ethiopia na vikosi vya Tigray yanawasukuma maelfu ya watu kukimbilia Sudan. 

Wafanyakazi wa UNHCR katika mpaka wa Hamdayet katika jimbo la Kassala na pia katika mpaka wa Lugdi katika jimbo la Gedaref wanaendelea kuwasajili maelfu ya wakimbizi wapya wanaowasili kila siku wengi wao wakiwa wamekimbia bila chochote isipokuwa vile walivyokuwa navyo tu na kisha wakilazimika kutembea kwa saa kadhaa na kuvuka mto kutafuta hifadhi nchini Sudan. 

Wakimbizi wanawasili katika maeneo ya mbali ambayo yana miundombinu michache mno. Mahitaji ya jumla ni makubwa, lakini kumekuwa na maendeleo kiasi katika kuyatimiza kwani msaada zaidi unafika kwenye mpaka. Jens Hesemann, Mratibu wa msaada wa dharura wa UNHCR Sudan anasema, "tuko hapa katika mpaka wa Hamdayet kati ya Sudan na Ethiopia. Kila siku maelfu ya wakimbizi wanakimbilia Sudan. Hali ni mbaya sana, na watu wanahitaji maji salama ya kunywa, wanahitaji chakula, wanahitaji malazi, wanahitaji kujisafi, wanahitaji huduma ya matibabu na msaada mwingine. UNHCR na washirika wake wako hapa kusaidia. Sasa tunahitaji msaada wa haraka wa wafadhili kusaidia shughuli hii ili tuweze kuleta mabadiliko katika kuokoa maisha kwa wakimbizi wa Ethiopia walioko Sudan.” 

Msemaji wa UNHCR atoa neno

UNHCR imepeleka wafanyakazi kutambua watu walio katika hatari zaidi yaani wenye mahitaji maalum. Vifaa zaidi vya matibabu vinafikia kliniki za afya ikiwemo chakula kilichoko tayari kwa matumizi.  Na ili kupambana na ugonjwa wa coronavirus">COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, kila anayeingia katika kituo cha afya cha kuhudumia watu wenye mahitaji maalum, anatakasa mikono.

Msemaji wa UNHCR, Babar Baloch akizungumza na wanahabari hii leo mjini Geneva Uswisi amesema hivi sasa chakula kinatolewa watoto wapatao 300 wenye utapiamlo na pia wanawake wajawazito pamoja na wale wanaonyonyesha.  

 “Tunaendelea kuhamisha wakimbizi mbali na mpaka na kutokana na mipango na umbali inaathiri idadi ya watu tunaoweza kuwasafirisha hadi kilomita 70 ndani ya Sudan katika eneo la Um Rakuba. Hadi kufikia jana Jumatatu, zaidi ya watu 8,000 walikuwa wamehamishwa.” Amesema Babar Baloch. 

Ndani ya Ethiopia, UNHCR bado ina wasiwasi kuhusu raia, pamoja na watu waliofurushwa pamoja na wafanyakazi wa misaada huko Tigray. UNHCR imesema inajiunga na washirika wa Umoja wa Mataifa katika kuzitaka pande zote zilizoko katika mzozo kufuata wajibu wao wa kimataifa kulinda raia.  

Aidha Baloch amesema katikati ya mzozo unaoendelea huko Ethiopia, wasiwasi pia unaongezeka kwa wakimbizi 100,000 wa Eritrea. Bila upatikanaji wa misaada, kuna wasiwasi mkubwa kuhusu utoaji wa huduma za msingi zaidi ikiwa ni pamoja na maji, dawa muhimu na usambazaji wa chakula, ambazo zitaisha kwa wiki moja kwa idadi ya wakimbizi.