Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzuia mauaji ya kimbari ni jukumu la jamii nzima :UN 

Manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa ni mwaka 1998  wakati wakiwa kwenye eneo la Mwurire nchini humo ambako kulifanyika mauaji.
UN/Milton Grant
Manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa ni mwaka 1998 wakati wakiwa kwenye eneo la Mwurire nchini humo ambako kulifanyika mauaji.

Kuzuia mauaji ya kimbari ni jukumu la jamii nzima :UN 

Haki za binadamu

Kuanzia majukwaa ya mitandao ya kijamii, makampuni ya teknolojia, viongozi wa kidini , viongozi wa asasi za kiraia na hata jamii nzima wote wana jukumu kubwa katika kupambana na kauli za chuki ambazo ni ishara ya wazi ya mauaji ya kimbari, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Antonio Guterres akizungumza leo katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya kuwaenzi waathirika wa mauaji ya kimbari na kukumbusha utu wao amesema ,“kuzuia mauaji ya kimbari kunahusisha jamii nzima na kuna haja ya kuongeza bidii kubadili hulka zilizotawala ambazo zinaathiri jamii zetu za leo.” 

Ameongeza kuwa janga la corona au coronavirus">COVID-19 limedhihirisha hali ilivyo tete katika jamii zetu na kuongeza changamoto za amani na usalama ambazo tayari zilikuwepo. 

Amerejea wito wa wa usitishaji uhasama kimataifa na kulitaka Baraza la Usalama kufanya kila liwezekanalo kuelekea utimizaji wa lengo hilo ifika[po mwisho wa mwaka huu. 

Pia Katibu Mkuu amesema, “mauaji ya kimbari huipa dunia mshituko mkubwa yanapotokea, lakini hayatokei bila kuwepo na ishara ninyi bayana. Waathirika mara nyingi ni walengwa wa awali wa kauli za chuki, ubaguzi na machafuko.” 

Tuwe makini kila wakati 

Bwana. Guterres amesisitiza haja ya kuwa makini kila wakati kuhusu mambo yanayoendelea kote duniani ya kisiasa, haki za binadamu, ya kibinadamu, kijamii na kiuchumi ili kubaini hatari za awali za mauaji ya kimbari na uhalifu mwingine wa kinyama. 

Ameonya kwamba uwezo wa mitandao ya kijamii, “katika kusambaza kauali za chuki na kusambaratisha jamii hauwezi kutopewa uzito. Hivyo ni muhimu sana kujikita na mikakati ya kitaifa, kikanda na kimataifa ya kuzuia mauaji hayo ambayo itashughulikia hususan uchochezi wa machafuko dhidi ya makundi na watu binafsi.” 

Katibu Mkuu pia amekumbusha kwamba ni muhimu kuhakikisha kuna mfumo thabiti wa uwajibikaji, "ni muhimu kwamba wote tunashikamana kutetea misingi ya usawa na utu wa binadamu.” 

Mkataba wa kuzuia mauaji ya kimbari 

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Volkan Bozkir kwa upande wake amesema, miaka 72 iliyopita mkataba wa kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari ulikuwa mkataba wa kwanza wa haki za binadamu kupitishwa na Baraza kuu. 

Na nchi 152 hivi sasa ni wanachama wa mkataba huo na amezichagiza nchi zilizoslia kuuridhia au kujiunga na mkataba huo na kutimiza wajibu wao katika kuzuia na kuhakikisha uwajibikaji wa uhalifu huo. 

Bozkir amesema, “licha ya uungwaji mkono mkubwa wa mkataba huo dunia ilishindwa kuzuia mauaji ya kimbari ya Rwanda , Sebrenica na Cambodia , Pamoja na hali nyingi za hivi karibuni za migogoro, vita na machafuko.” 

Ameongeza kuwa,”mauaji ya kimbari yana athari kubwa kwa waathirika na jamii ambazo zinachukua kama si miaka basi vizazi kuzikabili. Uwajibikaji na mifumo ya upatikanaji wa haki ina jukumu muhimu katika kuwasaidia waathirika na jamii kuponya majeraha ya athari hizo. Na ili kuwaenzi kikamilifu waathirika wa uhalifu huu mbaya zaidi, wahusika lazima wabainiwe, wakamatwe na kushitakiwa.” 

Kuzuia uhalifu huu ni wito wa UN 

Naye Alice Wairimu Nderitu mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari katika mkutano huo amesema, “kuzuia uhalifu wa mauaji hayo ni moja ya wito mkubwa na muhimu kwa Umoja wa Mataifa. Mauaji ya kimbari yamesababisha hasara kubwa kwa utu wa binadamu na jumuiya ya kimataifa ni lazima ifanye kila kitu kuhakikisha inazuia mauaji hayo na kuwalinda watu walio hatarini.” 

Bi. Nderitu amesema wakati uhalifu wa mauaji ya kimbari unapotekelezwa athari zake zinagusa hata nje ya mipaka na huenda zikawa ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa. 

Amesisitiza kwamba ongezeko kubwa la watu waliotawanywa na wakimbizi kutoka katika maeneo yenye vita na machafuko ni lazima likomeshwe mara moja kwani limesababisha madhara ya kibinadamu na kiuchumi yanatakayodumu kwa miongo. 

Mshauri huyo maalum ameonya kwamba, “kumekuwepo na ongezeko la machafuko ya itikadi kali yanayochagizwa kwa misingi ya kikabila au kidini katika nchi nyingi kote duniani mathalani Ethiopia, Myanmar, Sudan Kusini, Iraq na Syria na linachangia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaowakabili makundi mbalimbali ya kikabila, kidini na kitaifa sehemu mbalimbali duniani na hili halivumiliki.” 

Ameongeza kuwa, "baadhi ya mitazamo na mikakati ya kitaifa inachochea ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, ubaguzi mwingine na hali ya kutovumiliana duniani kote, katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea kidemokrasia na katika baadhi ya nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini. Hapa Marekani wimbi kubwa la maandamano lililoshuhudiwa hivi karibuni limekuwa ishara ya ubaguzi wa rangui ambao umeathiri mamilioni ya watu wenye asili ya Afrika kote duniani.” 

Bi. Nderitu amekumbusha kwamba mauaji ya kimbari hayatokei ghafla bali ni mchakato wenye dalili bayana. Amesisitiza haja ya kuchukua hatua mapema kukabiliana na hatari na kuchukua hatua za Pamoja kuhakikisha waathirika wanapata ukweli, haki na fidia.