Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wangu kwa wanangu, “Katu sitowasahau,” : Manusura mauaji ya Rwanda

Immaculée Songa, manusura wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya watutsi nchini Rwanda akiwa mbele ya maonesho yanayofanyika Umoja wa Mataifa. Gauni hilo ni la mtoto wake aliyeuawa wakati wa mauaji.
ONU Info/Florence Westergard
Immaculée Songa, manusura wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya watutsi nchini Rwanda akiwa mbele ya maonesho yanayofanyika Umoja wa Mataifa. Gauni hilo ni la mtoto wake aliyeuawa wakati wa mauaji.

Ujumbe wangu kwa wanangu, “Katu sitowasahau,” : Manusura mauaji ya Rwanda

Amani na Usalama

Immaculée Songa Mukantaganira, manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuelekea kumbukizi ya miaka 29 tangu mauaji ya kimbari nchini Rwanda anasema, “nguo hizo zinanipatia taswira ya mwisho ya binti zangu, jinsi maisha yao yalivyofupishwa, jinsi walikuwa watoto na malaika.”

Bi. Mukantaganira amezungumza na Florence Westergard wa Idhaa ya Kifaransa ya Umoja wa Mataifa kando mwa maonesho ya yanayofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, yakipatiwa jina Simulizi za kuishi na kukumbuka; Wito wa kuchukua hatua kuzuia mauaji ya halaiki.

Maonesho haya yamebeba kumbukizi za manusura wa uhalifu. Mauaji ya holokosti, halaiki na ukatili unaohusiana nao nchini Cambodi, mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 dhidi ya watutsi, mauaji ya kimbari huko ya mwaka 1995 huko Screbenica, Bosnia na Herzegovina.

Mauaji ya kimbari nchini Rwanda yalifanyika kwa siku 100 kuanzia Aprili 7 hadi Julai 15 mwaka 1994. Hadi leo hii manusura na wale waliopoteza ndugu na jamaa zao bado machungu yako moyoni mwao na wanatumia maonesho haya kupata sauti

Manusura wakiwemo Bi. Mukantaganira wanaonesha vitu mbalimbali vya kwao au vya jamaa zao na kuelezea vina maana gani.

Immaculée Songa, manusura wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya watutsi nchini Rwanda akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
ONU Info/Video
Immaculée Songa, manusura wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya watutsi nchini Rwanda akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Tazama jinsi gauni bado lina madoa ya damu licha ya kufuliwa

Mathalani kwenye maonesho hapa ni gauni la binti yake Raissa Umotoni wakati huo akiwa na umri wa miaka 3, halikadhalika gauni na fulana ya binti yake mwingine Clarisse Uwonkunda ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka mitano. Pia kuna kitabu cha picha za familia.

Nguo hizi ni muhimu sana kwangu, halikadhalika vifaa vingine vilivyoko kwenye maonesho haya, anasema Bi. Mukantaganira akiongeza kuwa kwa sababu vinatukumbusha maisha ya wale ambao hawako tena hapa na kwa kuwa hawako tena hapa, sisi ndio tunapaswa kusimulia historia zao na kwa vipi maisha yao yalichukuliwa.

Anaendelea kusema unaona madoa ya damu kwenye hizi nguo ijapokuwa zimefuliwa, hivyo hebu fikiria vifo vyao vilikuwa vipi. Hii ni mbaya sana kwa jamii.

Nilipoteza watoto wawili, mume, ndugu na jamaa

Katika mauaji hayo ya kimbari, Bi. Mukantaganira alipoteza mume wake, binti zake wawili na jamaa na marafiki wengi. Na katika mahojiano haya ametuma ujumbe wake kwa binti zake akisema katu hajawasahau na zaidi ya yote..

Mimi ni mama ambaye sijafa, mwanamke ambaye ninalia mno. Ninajiambia lazima kuna sababu Mungu aliniokoa na kunipatia nguvu ya kuzungumza juu yao badala ya kuacha wasahaulike.

Alipoulizwa juu ya umuhimu wa maonesho hayo, manusura huyu wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda anasema,

Immaculée Songa, manusura wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya watutsi nchini Rwanda akiwa mbele ya maonesho yanayofanyika Umoja wa Mataifa. Gauni hilo ni la mtoto wake aliyeuawa wakati wa mauaji.
UN News/Florence Westergard
Immaculée Songa, manusura wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya watutsi nchini Rwanda akiwa mbele ya maonesho yanayofanyika Umoja wa Mataifa. Gauni hilo ni la mtoto wake aliyeuawa wakati wa mauaji.

Vifaa hivi ni vithibitisho kwa wale wakanushao

Taarifa haziongopi. Kwa hiyo watu wakiona vithibitisho .. wakiona nguo za watoto wangu, hakuna kitu cha uongo. Watu wanasema watoto waliuawa, na hapa wataona ni ukweli.

Na zaidi ya yote amesisitiza kuwa mara kwa mara watu husikia takwimu za mamilioni ya watu waliuawa. Mfano watutsi nchini Rwanda waliouawa lakini  mtu mmoja mmoja anasahaulika kwa hiyo..Kwa hiyo maonesho haya yako pale ili tusisahau simulizi ya kila mtu, na kwa ujumla sasa inaitwa mauaji ya kimbari Rwanda. Hii inazungumza kwa sauti kubwa.

Wakati huu ambapo baadhi ya watu wanahaha kukanusha uwepo kwa mauaji ya kimbari, Bi. Mukantaganira anasema,

Chonde chonde kila mtu azuie mauaji ya kimbari

Serikali, watu wenye ushawishi na Umoja wa Mataifa wana wajibu wa kuzuia mauaji ya kimbari. Kwa upande wetu, nasi pia tunatimiza wajibu wetu. Mfano tunaandaa siku za kumbukizi na kuelimisha umma juu ya kile kinachoweza kutokea iwapo hawatakuwa makini. Kwa sababu mauaji ya kimbari yanaweza kuzuilika.