Tangu mauaji ya kimbari, Rwanda imeonesha kuwa inawezekana kunyanyuka kutoka katika majivu-Guterres

7 Aprili 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa ulimwengu mzima kujifunza kwa nchi ya Rwanda na watu wake kwa namna walivyomudu kuponya majeraha ya athari mbaya za mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi.

Ikiwa leo dunia inaadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi nchini Rwanda ambapo watu zaidi ya milioni moja waliuawa ndani ya siku 100, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , kupitia ujumbe wake wa video kuhusu siku hii ameanza kwa kusema kuwa siku hii inawaenzi wale wote waliouawa, wengi wakiwa watutsi pamoja na wahutu na watu wengine ambao waliyapinga mauaji ya kimbari. Bwana Guterres amesema, “na tunapata msukumo kutoka kwenye uwezo wa wale ambao walinusurika kwa kuwa na maridhiano na urejeaji katika maisha ya kawaida. Hatupaswi kamwe kuruhusu ukatili kama huo kutokea tena.”

Aidha Bwana Guterres amesema kuwa wanadamu wanapaswa  kusema hapana dhidi ya kauli za chuki na ubaguzi, na kukataa kujitenga, utaifa na uwekaji wa mipaka.

Katimu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kwa kutambua tu kwamba sisi sote ni familia moja ya wanadamu ndani ya sayari moja ndipo tutaweza kuzimudu changamoto nyingi za ulimwengu ambazo zinatukabili - kutoka kwa COVID-19 hadi mabadiliko ya tabianchi na kisha akasema, “tangu mauaji ya kimbari, Rwanda imeonesha kuwa inawezekana kunyanyuka kutoka katika majivu, kupona na kujenga upya jamii imara na iliyoendelevu zaidi. Tunapoangalia mbele kuongeza kasi ya juhudi za kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, wacha tuchukue funzo kutoka katika somo linaloendelea la Rwanda.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter