Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda nafuatilia kinachoendelea , jizuieni na ukiukwaji wa haki za binadamu:Guterres

Kutoka Maktaba: Abiria akiwa kwenye usafiri wa pikipiki maarufu kama Boda Boda mjini Kampaka nchini Uganda
© World Bank/Sarah Farhat
Kutoka Maktaba: Abiria akiwa kwenye usafiri wa pikipiki maarufu kama Boda Boda mjini Kampaka nchini Uganda

Uganda nafuatilia kinachoendelea , jizuieni na ukiukwaji wa haki za binadamu:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anafuatilia kwa karibu hali inayoendelea hivi sasa nchini Uganda na kusema anatiwa hofu na ripoti za machafuko na mauaji kufuatia maandamano yanayofanyika mjini Kampala.

Katika taarifa yake iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Ijumaa usiku mjini New York Marekani, Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kuwatakia ahuweni ya haraka wote waliojeruhiwa.

Katibu Mkuu amelaani vikali vitendo vyote vya machafuko na kutoa wito kwa mamlaka nchini Uganda kuhakikisha wahusika wote wa vitendo hivyo vya ukiukwaji wa haki za binadamu wanawajibishwa.

Pia ametoa wito wa kuachiliwa mara moja mtutu yeyote ambaye amekamatwa na kushikiliwa kinyume cha sheria. Bwana Guterres ametoa wito kwa vikosi vyote vya ulinzi na usalama nchini Uganda kuwajibika kwa kuzingatia utawala wa sheria na misingi ya haki za binadamu lakini pia kujizuia na machafuko yoyote.

Katibu Mkuu pia amewataka viongozi wote wa kisiasa na wafuasi wao kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kwa amani , kwa kuzingatia sheria na kujizuia na matukio yoyote ya machafuko au kauli za chuki.

Chanzo cha vurugu

 

Ka mujibu wa duru za Habari maelfu kwa maelfu ya watu wamekuwa wakiandamana mitaani kuunga mkono kampeni za uchaguzi za mgombea wa Urais wa upinzani nchini humo kupitia chama cha People’s Power,   mwanamuziki maarufu ajulikanaye kama Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamuu aliyechaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo baada ya kusimama kama mgombea huru mwaka jana wilayani Kyadongo Mashariki , katikati mwa Uganda.

Na sasa Bobi Wine anagombea urais dhidi ya Rais aliyeko madarakani hivi sasa Yoweri Kaguta Museveni katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi Januari mwaka 2021.

Kwa mujibu wa polisi wa Uganda chanzo cha machafuko yanayoendelea ni ukiukwaji wa mikakati ya kudhibiti kusambaa kwa janga la corona au coronavirus">COVID-19 ambayo inakataza mikusanyiko ya watu zaidi ya 200 katika mikutano na maandamano ya kampeni.

Polisi hao pia wamesema kati ya Jumatano na Alhamisi wiki hii watu 28 wamefariki dunia katika vurugu za maandamano japo vyombo vya Habari nchini humo vinanukuu vyanzo vya hospitali vikisema idadi ya waliopoteza maisha siku hizo mbili ni 37.