Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na wadau wahitaji dola milioni 45.5 kuwasaidia waathirika wa kimbunga Goni Ufilipino

Timu ya IOM wakiwa mashinani kutathimini mahitaji muhimu ya waathirika wa kimbunga Goni.
IOM
Timu ya IOM wakiwa mashinani kutathimini mahitaji muhimu ya waathirika wa kimbunga Goni.

UN na wadau wahitaji dola milioni 45.5 kuwasaidia waathirika wa kimbunga Goni Ufilipino

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wametoa ombi la dola milioni 45.5 ili kuwasaidia watu 260,000 katika maeneo yaliyoathirika zaidi na kimbunga Goni nchini Ufilipino.

Katika jimbo la Albay lililoko ufukweni mwa bahari nchini Ufilipino hali ni mbaya na ya kusikitisha kwani uharibifu ni mkubwa ulioletwa na kimbunga Goni ikiwemo vifo, kusambaratisha miumndombinu na kuwaacha maelfu ya watu bila makazi wala chochote. 

Chirica Guiba mwenye umri wa miaka 26 ni miongoni mwa watu waliopoteza kila kitu kwenye janga hili ikiwemo nyumba waliyokamilisha kujenga yeye na familia yake katika kitongoji cha Barangay Baybay jimboni humo na sasa wamejikuta hawana pa kuishi. “Nyumba yetu imesambaratishwa kabisa na kimbunga, ilikuwa mpya ndio imekamilika tu kujengwa, lakini sasa iko nyan’ganyan’ga hakuna kilichosalia. Ilikuwa na sebule na upande wa pili jiko lakini kama unavyoona yote imekwenda, hakuna kitu kilichobaki, hivyo hatuwezi kukaa hapa tena tunahitaji kuanza upya.” 

Kimbunga hicho kiliambatana na mvua kubwa, upepo mkali ulioezua paa za nyumba na kuangusha majengo lakini pia mafuriko na maporomoko ya udongo.  

Hivi sasa msaada umenza kuwafikia maelfu ya waathirika na mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Ufilipino Gustavo Gonzales ameongoza timu ya mashirika ya kibinadamu kwenda jimboni Albay kushuhudia hali halisi anasema,“Kitu cha kwanza ni kuelezea hofu yetu kwa mamlaka kuhusu athari kwa maisha ya watu. Miundombinu karibu asilimia 90 ya mifumo ya umeme imesambaratishwa na hofu yetu ni athari zake kwa watu. Tuko katikati ya janga la COVID-19 na kisha zahma hii, tukiangalia mazingira na tukiangalia athari inabidi tutambue kwamba tuko katika eneo ambalo kila wakati na kila mwaka linaathirika na kimbunga.” 

Amesema fedha zilizoombwa dola milioni 45.6 zaidi zitasaidia katika manispaa 16 zilizoathiriza vibaya kwenye majimbo ya Catanduanes na Albay sanjari na juhudi za serikali.