Mashirika ya UN yasaidia mamilioni ya waathirika wa kimbunga Goni Ufilipino

Waathirika wa kimbunga nchini Ufilipino wakiwasili mji mkuu Manila Novemba 1, 2020.
UNICEF/Larry Monserate Piojo
Waathirika wa kimbunga nchini Ufilipino wakiwasili mji mkuu Manila Novemba 1, 2020.

Mashirika ya UN yasaidia mamilioni ya waathirika wa kimbunga Goni Ufilipino

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu nchini Ufilipino wanashikamana ili kuzisaidia jamii zilizoathirika vibaya na kimbunga Goni ambacho kimekumba nchi nzima na kuacha uharibifu mkubwa. 

Kimbunga Goni ambachi kinajulikana nchini humo kama Rolly kiwalisi Ufilipino Jumapili asubuhi katika majira ya nchi hiyo kikiambatana na upepo mkali wa kilimota 280 kwa saa na mvua kubwa. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA, takriban watu milioni 68.6 wameathirika na kimbunga hicho huku watu milioni 24.3 kati yao wanaishi katika maeneo yaliyoathirika zaidi. 

Kati ya watu hao walioathirika zaidi milioni 2.3 ni wasio jiweza na walio hatarini na 724,00 kati yao ni watoto. 

Kufuatia kimbunga hicho kumeripotiwa mafuriko na uharibifu mkubwa wa miundombinu huku ripoti za awali zikisema watu 10 wamepoteza maisha akiwemo mtoto wa umri wa miaka 5 kwa sababu ya kuzama na kuangukiwa na kifusi. 

Gustavo Gonzalez mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ufilipino amesema kwamba wahudumu wa misaada hawqakusubiri kimbunga hicho kuwasili ili kujikusanya na kuchukua hatua. 

“Mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale yasiyo ya kiserikali NGO’s ya misaada ya kibinadamu tayari yanashirikiana na ofisi na idara za serikali , chama cha msalaba mwekundu cha Ufilipino na makundi ya sekta binafsi kuratibu kufanya tathimini ya haraka ya mahitaji na kutoa msaada kwa makundi yaliyohatarini zaidi kwanza ambayo yameathirika na uharibifu wa kimbunga hicho.” 

Jiandaeni na zahma zaidi 

Bwana Gonzalez pia ametoa wito kwa kila mtu kufuata na kuzingatia mwongozo unaotolewa na mamlaka. 

“Watu wa Ufilipino wana mnepo wa hali ya juu, lakini kimbunga hiki ni hatari kubwa , ni lazima tujiandae kwa zahma kubwa zaidi na kuwa tayari kuokoa maisha. Katika saa na siku zijazo ni lazima tufanye kila liwezekanalo kuokoa maisha na kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma” ameongeza afisa huyo wa Umoja wa Mataifa. 

Hatua zinazochukuliwa na UN 

Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa upandewake yanashiriki na kusaidia juhudi za serikali. OCHA ndiyo inayoratibu masuala ya kibinadamu na kuwapanga wadau wengine wa misaada na maendeleo katika maeneo yaliyoathirika ili kusaidia katika tathimini ya athari za kimbunga hicho. 

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM linaisaidia mamlaka nchini Ufilipino katika kusimamia vituo vya kuhamishia waathirika , huku shirika la mpango wa chakula duniani WFP limepewa ombi la msaada wa kiufundi hasa katika ugawaji wa chakula. 

Kwa upende wake Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF limeandaa misaada ya dharura kwa familia na liko tayari kutoa msaada wa kuokoa maisha.maisha ya Watoto, maendeleo na ulinzi wao. 

“Watoto ni miongoni mwa walio hatarini zaidi wakati wa dharura yoyote. Tunafuatilia kwa karibu hali na tunatiwa hofu na uhai, maendeleo na ulinzi wao. “ limesema shirika hilo na kuongeza kuwalinaweza kukusanya wadau haraka na wasambazaji endapo litahitajika.  

Wadau wa kitaifa pia wamejikusanya ili kufanya tathimini ya hali pamoja na kuisaidia serikali katika juhudu za uokozi na kutoa misaada ya dharura katika jamii zilizoathirika zaidi.