Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 368,000 wako hatarini Msumbiji baada ya kimbunga Kenneth:UNICEF

Baadhi ya  uharibifu  uliosababishwa na kimbunga Kenneth kilichopiga eneo la Pemba jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji tarehe 25 Aprili 2019
WFP/Maktaba ya Picha
Baadhi ya uharibifu uliosababishwa na kimbunga Kenneth kilichopiga eneo la Pemba jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji tarehe 25 Aprili 2019

Watoto 368,000 wako hatarini Msumbiji baada ya kimbunga Kenneth:UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limeonya kwamba watoto na familia zao nchini Msumbiji wanaweza kukabiliwa na hatari ya kifo kutokana na mafuriko makubwa na maporomoko ya udongo baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa WMO kuonya kwamba mvua kubwa itaendelea kunyesha. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatarajiwa kuzuru hivi karibuni nchini humo.

Kwa mujibu wa UNICEF watoto 368,000 hivi sasa wako hatarini nchini Msumbiji na wanaweza kuhitaji msaada wa kibidamu. Nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika juma hili imekumbwa na kimbunga cha pili Kenneth ikiwa ni wiki sita tu baada ya kimbunga Idai kusambaratisha mji wa Beira na viunga vyake na kusababisha uharibifu mkubwa ikiwemo kupotea kwa maisha ya watu na miundombinu.

Mamlaka nchini Msumbiji imethibitisha kwamba hadi kufikia sasa watu watano wamepoteza maisha kutokana na kimbunga Kenneth.

Makadirio

Kimbunga Kenneth kiliwasili Alhamisi wiki hii Cabo Delgado katika jimbo la Kaskazini mwa Msumbiji kikiwa na kasi ya daraja la 4 na watabiri wameonya kwamba mvua kubwa itaendelea kunyesha kwa siku kadhaa zijazo na kuyaweka katika hatari kubwa ya mafuriko na maporomoko ya udongo maeneo yaliyoathirika. UNICEF pia imesisitiza kwamba hofu kubwa kwa sasa ni watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine hasa ukizingatia kwamba kimbunga hicho kimeharibu asilimia 90 ya nyumba katika baadhi ya vijiji. Cabo Delgado haina historia ya vimbunga hivyo hofu ni ya haraka kwamba jamii katika eneo hilo hawajajiandaa na kiwango hicho cha kimbunga na hivyo kuwaweka Watoto na familia katika hatari kubwa.

Hali baada ya kimbunga Kenneth kupiga eneo la Pemba nchini Msumbiji jana tarehe 25 Aprili 2019
WFP/Maktaba ya Picha
Hali baada ya kimbunga Kenneth kupiga eneo la Pemba nchini Msumbiji jana tarehe 25 Aprili 2019

Msaada

Katika taarifa iliyotolewa na mwakilishi wa UNICEF nchini Msumbiji imeongeza kwamba udongo bado umejaa maji ya mvua na mito imefurika hivyo hali huenda ikawa mbaya zaidi kutokana na mafuriko katika siku zijazo na amewahakikishia watu wa maeneo husika kwamba UNICEF inafanya kila iwezalo ili kupeleka timu na rasilimali zinazohitajika kuhakikisha watu hao wako salama. Shirika hilo pia limearifu kwamba tayari lina timu Cabo Delgado ambayo ina wataalm wa afya, lishe, ulinzi wa watoto, maji na usafi na inagawa misaada ya kibinadamu. UNICEF hivi sasa inatathmini hali ili kubaini ukubwa wa janga hilo katika siku zijazo. Hii ni mara ya kwanza katika historia kwamba vimbunga viwili vikubwa kuikumba Msumbiji katika msimu mmoja.

Ombi

Kimbunga Kenneth kimefuata nyayo za kimbunga Idai ambacho kimekatili maisha ya watu zaidi ya 600. Kwa mujibu wa UNICEF zahma iliyosababishwa na vimbunga hivyo viwili vinaweza kuwafanya Watoto milioni 1.4 kuhitaji msaada wa kibinadamu katika eneo la Kaskazini na katikati mwa Msumbiji. Kufuatia kimbunga Idai kilichotokea mwezi Machi UNICEF imezindua ombi la dola milioni 122 ili kutoa msaada wa mahitaji ya kibinadamu kwa Watoto na familia zao walioathirika na kimbunga hicho Msumbiji, Zimbabwe na Malawi kwa miezi tisa ijayo.