Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na serikali ya Kenya wazindua mpango usaidizi wa kifedha kwa familia zilizoathiriwa na COVID-19 Mombasa, Kenya

Familia 24,000 nchini Kenya mji wa Mombasa wamepokea pesa taslimu kutoka kwa WFP kufuatia vipato vyao kusambaratishwa na COVID-19
WFP
Familia 24,000 nchini Kenya mji wa Mombasa wamepokea pesa taslimu kutoka kwa WFP kufuatia vipato vyao kusambaratishwa na COVID-19

WFP na serikali ya Kenya wazindua mpango usaidizi wa kifedha kwa familia zilizoathiriwa na COVID-19 Mombasa, Kenya

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP kwa kushirikiana na serikali ya Kenya leo wamezindua mpango wa ugawaji fedha taslim kwa familia 24,000 mjini Mombasa, Kenya katika makazi yasiyo rasmi ambao maisha yao yamesambaratishwa na athari za janga la COVID-19.

Mipango ya kudhibiti janga hilo la virusi vya corona ikiwemo vizuizi vya kusafiri nje na kwa kiasi fulani vizuizi vya kuzunguka ndani ya nchi vimesababisha athari kubwa za kiuchumi hasa kwa watu wa Pwani ambao wanategemea pato la kila siku katika sekta zisizo rasmi na utalii. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na WFP mjini Mombasa hii leo, Kaunti ya Mombasa ina asilimia 12 ya idadi ya wagonjwa wa COVID-19 nchini Kenya ambayo ni idadi ya pili kwa ukubwa baada ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Utalii ulikuwa chanzo kikuu cha mapato katika kaunti ya Mombasa kabla ya janga hilo. Kutokana na  matokeo ya kuongezeka kwa maambukizi, sehemu kubwa ya sekta ya utalii ililazimika kupunguza wafanyakazi wake na biashara nyingi zilifungwa kabisa au zinahangaika kuendelea kuwepo. 

Pesa taslimu zimesambazwa kwa famila zilizoathirika na COVID-19 Mombasa, Kenya.
WFP/David Orr
Pesa taslimu zimesambazwa kwa famila zilizoathirika na COVID-19 Mombasa, Kenya.

Mnamo tarehe mosi mwezi Septemba mwaka huu, Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya ilikadiria kwamba Wakenya wapatao milioni 1.7 walipoteza kazi kote nchini humo. Kiwango cha ukosefu wa ajira kiliongezeka mara mbili hadi asilimia 10.4 ikilinganishwa na asilimia 5.2 mnamo Machi wakati maambukizi ya kwanza ya COVID-19 yaliporitiwa. 

Kwa msingi huo, WFP pamoja na mchango kutoka Ofisi ya Usaidizi wa Kibinadamu ya shirika la Marekani la msaada wa kimataifa USAID, imezindua msaada wa kuokoa maisha  kwa familia 24,000 au sawa na watu 96,000  kwa namna moja au nyingine vipato vyao vimeathiriwa na mlipuko wa virusi vya corona katika Mombasa.  

Mkurugenzi wa WFP nchini Kenya Lauren Landis amesema, “COVID-19 imesababisha mateso yasiyotarajiwa hasa kwa familia zinazoishi katika maeneo duni ya miji ambao kwa kawaida hutegemea ajira isiyo rasmi ya kila siku. Familia nyingi katika eneo la pwani wanajitahidi kujilisha wenyewe. Msaada wa WFP unaongezea kwenye mipango mingine ya ulinzi wa jamii unaoendeshwa na serikali za kitaifa na kaunti. Kwa pamoja, tunaweza kuepusha shida ya njaa na lishe kati ya jamii maskini zinazoishi mijini.”  

Taarifa ya WFP imeeleza kuwa, mara moja kwa mwezi, kila familia iliyochaguliwa itapokea shilingi 4,000 za Kenya sawa na dola 40 za Kimarekani  za kutosha kugharamia nusu ya mahitaji ya kila mwezi ya chakula na lishe kwa familia ya watu wanne. Fedha na msaada wa lishe ya ziada kwa wanawake na watoto zitatolewa kwa miezi mitatu. 

Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Hassan Ali Joho amenukuliwa akisema, “tunakaribisha msaada kutoka na WFP na USAID. Msaada huu utasaidia sana kuzihifadhi familia nyingi zilizo katika shida kufuatia upotezaji wa mapato kutokana na vizuizi vya COVID-19.”