Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN imelaani vikali shambulio la kutumia kisu ndani ya kanisa Ufaransa 

Mjini Nice Ufaransa ambako tukio linalodaiwa kuwa la kigaidi limefanyika ndani ya kanisa katikati ya mji 29 Oktoba, 2020
Unsplash/Roxana Crusemire
Mjini Nice Ufaransa ambako tukio linalodaiwa kuwa la kigaidi limefanyika ndani ya kanisa katikati ya mji 29 Oktoba, 2020

UN imelaani vikali shambulio la kutumia kisu ndani ya kanisa Ufaransa 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Msataifa leo amelaani vikali shambulio la kisu lililofanyika ndani ya kanisa kwenye mji wa Kusini  wa Nice nchini Ufaransa ambalo limesababisha vifo vya waumini watatu. 

Katika taarifa iliyotolewa hii leo jijini New York, Marekani na msemaji wake , Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na kusisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa kwa watu na serikali ya Ufaransa. 

Duru zinasema mshambuliaji mmoja aliyekuwa amejihami kwa kisu aliingia katika kanisa mashuhuri la Notre Dame Basilica lililopo katikati ya mji majira ya saa tatu asubuhi saa za Ufaransa na kutekeleza shambulio hilo. 

Mwanaume mmoja na mwanamke mmoja walikufa papo hapo wakati mwanamke mwingine alikufa baadaye kutokana na majeraha aliyoyapata na mshambuliaji alijeruhiwa baada ya kupigwa risasi na polisi na kisha akapelekwa hospitali. 

Serikali ya Ufaransa imesema inalichukulia shambulio hilo kama tukio la kigaidi. 

Mashambulizi Ufaransa na Saudia 

Shambulio hilo la mauaji ya kikatili mjini Nice sio tukio pekee lililotokea leo kufuatia hatua ya Ufaransa ikiongozwa na Rais Emmanuel Macron kufuatia mauaji ya mwalimu aliyekatwa kichwa karibu na mji wa Paris yapata wiki mbili zilizopita. 

Shambulio hilo limeelezwa kufanyika kujibu hatua ya kuchapisha vibonzo vilivyomdhalilisha au kumkashifu Mtume Mohammed S.A w kwenye jarida la Charlie Hebdo. 

Pia kumekuwa na taarifa ya mwanaume mmoja kupigwa risasi na kuuawa karibu na mji wa Avignon Kusini mwa Ufaransa baada ya kuripotiwa kumtishia polisi kwa bastola. 

Na kwa mujibu wa duru za habari, mlinzi wa ubalozi wa Ufaransa mjini Jeddah Saudi Arabia alishambuliwa leo na kujeruhiwa na polisi walifanikiwa kumkamata mshukiwa. 

Kufuatia mauaji hayo ya Nice, polisi nchini Ufaransa wameanzisha uchunguzi wa mauaji huku Rais Macron akiliita shambulio hilo kuwa shambulio la kigaidi la kiislam huku tahadhari ya kitaifa ya usalama ikiwa imepandishwa katika kiwango cha juu. 

Baada ya mauaji ya mwalimu Samuel Paty na Rais Macron kutetea uchapishaji wa vibonzo vya mtume Muhammed, kumekuwa na maandamano katika baadhi ya nchi za Kiislam kwa kile kinachoolezwa ni ya dhidi ya kupinga Uislam na wito umekuwa ukitolewa wa kugomea bidhaa za Ufaransa, ikiwamo kutoka kwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. 

Hali ya kuvumiliana inahitajika 

Katika taarifa yake kufuatia mauaji hayo ya Nice afisa wa Umoja wa Mataifa anayehusika na kusimamia ulinzi wa maeneo ya kidini na kuchagiza kuvumiliana katika masuala ya kidini Miguel Aingel Moratinos amelaani vikali shambulio hilo la kinyama na kusisitiza kwamba , shambulio lolote linalolenga raia, ikiwemo waumini halivumiliki na halihalalishwi popote, kwa njia yoyote ile na kwa yeyote yule anayelitekeleza.