Nalaani vikali shambulio la leo Ouagadougou:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres akihutubia Baraza la Usalama.
UN /Loey Felipe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Baraza la Usalama.

Nalaani vikali shambulio la leo Ouagadougou:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la leo mjini Ouagadougou nchini Burkina Fasso, dhidi ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo na ubalozi wa Ufaransa.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Guterres amezungumza kwa njia ya simu na rais wa nchi hiyo  Roch Marc Christian Kaboré, na kuonyesha mshikamano wake na serikali na watu wa  Burkina Faso.  

Ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi.  Kwa mujibu wa duru mbalimbali za habari wanajeshi wanane na washambuliaji wanane wameuawa na watu 80 kujeruhiwa wakiwemo raia katika shambulio hilo linalodaiwa kuwa la kigaidi.

Katibu Mkuu ameichagiza serikali ya Burina Fasso kuanzisha uchunguzi dhidi ya mashambulio hayo na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria.

Pia amerejelea ahadi kwamba Umoja wa Mataifa umejizatiti kuisaidia Burkina Fasso katika juhudi zake za kupambana na ghasia za itikadi kali na ugaidi, kufanya mabadiliko katika sekta ya usalama, kuchagiza maridhiano ya kitaifa na kuweka mazingira muafaka kwa ajili ya amani ya kudumu na maendeleo.

Guterres pia ametoa wito wa juhudi za haraka na za pamoja za jumuiya ya kimataifa kusaidia nchi katika kanda kukabiliana na changamoto za amani na usalama, maendeleo na masuala ya kibinadamu zinazoathiri eneo la Sahel, ikiwa ni pamoja na kupitia mkakati wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sahel na utendaji kamili wa jeshi la pamoja la kanda ya Sahel yaani G5.