Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Linapokuja suala la amani, kuzuia migogoro ni bora kuliko kuikabili:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kongamano la amani la Paris nchini Ufaransa
@ UNESCO/Christelle Alix
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kongamano la amani la Paris nchini Ufaransa

Linapokuja suala la amani, kuzuia migogoro ni bora kuliko kuikabili:Guterres

Amani na Usalama

Kuzuia vyanzo vote vinavyosababisha uvunjifu wa amani duniani ndio dawa mujarabu ya kulinda na kudumisha amani ya dunia kuliko kukabili machafuko wakati yameshatokea. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mjini Paris Ufanransa hii leo, wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la Paris kwa ajili ya amani.

Guterres amesema mafanikio makubwa na ya haraka ya kongamano hilo ni kusisitiza haja ya kuwa na mtazamo mpya kuhusu utawala wa kimataifa. Watu wakikumbuka karne moja tangu vita kuu ya kwanza ya dunia na walichojifunza kutokana na athari zake.

Ameongeza kuwa ingawa ukilinganisha na migogoro mikubwa ya karne zilizopita hali ya sasa inaonekana kuwa ni ya amani zaidi, lakini ukweli ni kwamba “Bado tuko mbali kuwa na ile tunayoiita amani ya kweli, hali halisi ni ya sintofahamu na changamoto kubwa. Ukiangalia Sahel, Libya, Syria, Yemen, Afghanistan kote duniani migogoro inaendelea, inasababisha madhila na kukatili maisha ya watu, dunia yetu iko katika zahma kubwa. Sio tena suala la fikra moja au la kikundi, lakini bado hatujafikia fikra za pamoja. Uwiano wa mamlaka hautabiriki.”

Tishio lililopo

Guterres amesema mara nyingi sio suala la vita baina ya mataifa, bali migogoro ambapo mataifa yanakabiliwa  na makundi yasiyo ya kitaifa. Na kuongezeka kwa kuingiliwa na upande wa tatu , migogoro hii inachukua mtazamo wa kikanda. Na wakati huohuo uhusiano baina ya mataifa yenye nguvu hivi sasa umesambaratika kuliko wakati mwingine wowote. “Tunashuhudia athari za kujutia kwa baraza la Usalama ambalo mara kwa mara linakoseshwa nguvu. Na hata wakati Baraza linachukua hatua uingiliwaji toka nje unafanya utekelezaji wa maazimio kuwa mgumu zaidi. Angalia vikwazo vya silaha vya Libya , hakuna mtu anayeheshimu na hatuwezi hata kujaribu kuficha, na mivutano ya ndani au ya kikanda inazidi kusambaa.”

Ongezeko la machafuko na vita

Katibu Mkuu amesema hivi sasa migogoro inaendelea kutegemeana na kuhusiana na mfumo mpya wa ugaidi wa kimataifa. Kwa mfano amesema athari za mgogoro wa Libya kwa eneo la Sahel na ukanda wa ziwa Chad ni jambo la kusikitisha. Mbali ya hayo ametaja hatari ya uzalishaji wa nyuklia ambao uko mbali kutoweka  na unarejea kwa nguvu zote. Kwa mantiki hiyo amesema ‘’kuzuia ni bora zaidi  na muhimu hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Ni lazima tushughulikie mizizi yake na kuzuia kuongezeka kwa mivutano au kulipuka kwa vita vipya. Hili litawezekana kwa misingi ya ushirikiano wa kimataifa.’’

Amesisitiza kwamba hii ndio maana amezindua mkakati wa mabadiliko kwenye mfumo wa Umoja wa Mataifa ambao unaweka suala la kuzuia migogoro na upatanisho katika kitovu cha shirika hili wakati ukiandaliwa mfumo wa kukabiliana na machafuko ya itikadi kali na kuimarisha  amani na usalama wa kimataifa kwa ushirikiano na mashirika ya kikanda kama vile Muungano wa afrika na Muungano wa Ulaya.

Hatari tano zinazoikabili dunia hivi sasa

Katika ulingo wa kimataifa Guterres ametaja hatari tano zinazoikabili dunia hivi sasa akisema Mosi, tunaona hatari ya mgawanyiko wa kiuchumi, kiteknolojia na kijiografia.

Sayari iliyogawanywa mapande wmawili yenye nguvu kubwa za kiuchumi yakianzisha nguvu zao juu ya dunia mbili tofauti katika mashindano, kila moja na msimamo wake, sheria zake za kibiashara na kifedha, mtandao wake mwenyewe intaneti, maendeleo yake ya akili bandia na yenyewe mikakati yake ya kijiografia na kijeshi kwa  jumla. Tunapaswa kufa kila liwezekanalo kuzuia mgawanyiko huu na mkubwa na kulinda mfumo wa kimataifa, uchumi wa dunia kwa minajili ya sheria za kimataifa , ushirikiano wa pamoja na taasisi imara za pamoja.

Na katika hili tunahitaji Ulaya iliyo imara kama nguzo ya ushirikiano wa kimataifa kutokana na utawala wa sheria na kuheshimu misingi ya uhuru.

Pili Katibu Mkuu amesema wakati huohuo tunapaswa kuangalia katika ngazi ya kitaifa mgawanyiko wa kijamii na tofauti zilizopo.

Tatu tunashuhudia wimbi la maandamano kote duniani, na kama kila hali ni tofauti basi amesema kuna mambo mawili ambayo yanashabihiana.

Kwanza kabisa tunashuhudia ongezeko la kutoaminiana baina ya raia na taasisi za kisiasa na viongozi, usawa wa kijamii uko katika tisho kubwa. Pili tunashuhudia athari za utandawazi unaohusiana na maendeleo ya kiteknolojia zikiongeza pengo la usawa katika jamii.

Nne watu wanataabika sana na wanataka kusikilizwa, wana kiu ya kupata usawa. Wanadai kuwa na mfumo wa kijamii na kiuchumi ambao unafanyakazi kwa maslahi ya wote.

Na tano wanataka haki zao za binadamu na uhuru wa msingi vitekelezwe na kuzingatiwa kwa wote.