Shule hazipaswi kulengwa na mashambulizi Pakistan: UNICEF  

27 Oktoba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limelaani vikali shambulio la mabomu lililokatili maisha ya angalau watu saba kwenye shule ya kidini nchini Pakistan. 

Akisistiza kutolenga shule kufuatia shambulio hilo la leo Aida Girma mwakilishi wa UNICEF nchini Pakistan amesema “Elimu ni haki ya msingi ya kila msichana na mvulana kila mahali. Shule asilani hazipaswi kulengwa na mashambulizi.” 

Kwa mujibu wa duru za Habari mlipuko huo wa bomu uliilenga shule ya dini au madrassa ya Jamia Zuberia katika mji wa Dir Colony eneo la Peshawar wakati wanafunzi wakiwa madarasani wanasoma. 

Taarifa za karibuni zinasema zaidi ya watu 130 wamejeruhiwa na wengi wao ni kati ya wanafunzi 500 au Zaidi walioutana kwa ajili ya muhadhara shuleni na wengi wao wakiwa na umri wa kati ya miaka 20 na 30. 

Bi. Girma amesisitiza kwamba “Shule lazima ziwe ni mazingira salama ya kusoma kwa wakati wote kwa ajili ya kulinda ukuaji na maendeleo ya afya ya Watoto, barubaru na vijana.” 

UN yaomboleza na taifa hilo 

Kupitia ukurasa wake wa twitter hii leo osifi ya Umoja wa Mataifa nchini Pakistan imesema “Tuko Pamoja katika mshituko na majonzi baada ya shambulio la kikatili na la kutisha kwenye madrassa ya Jamia Zubairia huko Peshawar ambako watoto walikuwa madarasani. Tumesikitishwa na shambulio hili dhidi ya Watoto wakiwa katika eneo la sala na kujifunza.Tunatoa salamu za rambirambi kwa waathirika na familia zao.” 

Peshawar ni mji mkuu wa jimbo la Khyber Pakhtunkhwa linalopakana na Afghanista. 

Hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kutekeleza unyama huo. Hata hivyo kwa mujibu wa duru za Habari kundi la Taliban nchini Pakistan limetoa taarifa kukana kuhusika kwa aina yoyote na shambulio hilo na limelaani kulenga shule za kidini na kusema ni kitendo cha kikatili. 

Shambulio la leo limekuja siku mbili tu baada ya shambulio la bomu kwenye mji wa Quetta Kusini Magharibi mwa nchi hiyo kukatili Maisha ya watu watatu. 

UNICEF imesema mwaka 2018 kulikuwa na mfululizo wa mashambulizi katika shule mbalimbali nyingi zikiwa ni za wasichana katika eneo la Gilgit-Baltistan wilaya ya Diamer na pia shule ilishambuliwa katika eneo la Chitra. 

Desemba mwaka 2014 wapiganaji wa kigaidi kutoka nje walishambulia shule ya umma ya kijeshi mjini Peshawar na kuuwa karibu wafanyakazi na watoto 150. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter