Shule nyingi duniani hazina maji safi na salama ya kunywa- Ripoti

Watoto nchini Sudan Kusini wakiwa wamepanga foleni ili kupata maji ya kunywa kwenye kituo cha Umoja wa Mataifa cha ulinzi wa raia huko mjini Malakal nchini Sudan Kusini.
© UNICEF/Sebastian Rich
Watoto nchini Sudan Kusini wakiwa wamepanga foleni ili kupata maji ya kunywa kwenye kituo cha Umoja wa Mataifa cha ulinzi wa raia huko mjini Malakal nchini Sudan Kusini.

Shule nyingi duniani hazina maji safi na salama ya kunywa- Ripoti

Afya

Je shule anayosoma mwanao ina huduma za maji ya kunywa na vyoo? Au je shule uliyosoma iwe  ya awali, msingi au sekondari ilikuwa na huduma hizo muhimu za msingi? Ripoti ya kwanza kabisa inayofuatialia huduma hizo inaonyesha hali mbaya na ya kusikitisha. Kuna shule za msingi hazina kabisa vyoo, maji wala huduma za kujisafi.

Wiki ya maji ikiingia siku ya pili hii leo, imeelezwa kuwa asilimia 69 ya shule ulimwenguni kote hazina huduma ya maji ya kunywa, imesema ripoti ya kwanza ya mashirika ya Umoja wa Mataifa iliyoangazia makadirio ya upatikanaji wa maji ya kunywa, huduma za kujisafi na usafi shuleni.

Takwimu za ripoti hiyo iliyotolewa leo na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa,  UNICEF na lile la afya, WHO zinaonyesha kuwa shule moja ya msingi kati ya nne haina kabisa huduma ya maji ya kunywa na hali inakuwa mbaya zaidi kwa shule za sekondari ambapo ni shule moja kati ya sita tu ndio yenye maji ya kunywa.

Kwa upande wa vyoo, ripoti inasema ni asilimia 66 tu ya shule ulimwenguni kote ndio zilikuwa na vyoo mwaka 2016 ambapo kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara pamoja na Ocenia theluthi moja ya shule hazina kabisa vyoo.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mtoto akinawa  mikono katika moja ya maeneo ya shule ambako wamewekewa huduma hiyo na UNICEF
UNICEF/Jonathan Shadid
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mtoto akinawa mikono katika moja ya maeneo ya shule ambako wamewekewa huduma hiyo na UNICEF

Akizungumzia ripoti hiyo Kelly Ann Naylor, ambaye ni Mkuu wa huduma za maji, kujisafi na usafi UNICEF amesema iwapo elimu ni ufunguo wa kumsaidia mtoto kuondokana na umaskini, basi kupata maji safi, na huduma za kujisafi ni ufunguo wa kumwezesha mtoto kunufaika zaidi na elimu.

Shule zinapokuwa na maji safi, vyoo na sabuni za kunawa mikono watoto wanakuwa na mazingira salama ya kujifunzia, na mahudhurio ya wanafunzi wa kike yanakuwa bora zaidi kwa kuwa wanaweza kufika shuleni hata wakati wa hedhi.

“Kupuuza hili ni kutojali ustawi na afya ya mtoto,” amesema Bi. Naylor.

Bi. Naylor amesema shule zinapokuwa na maji safi, vyoo na sabuni za kunawa mikono watoto wanakuwa na mazingira salama ya kujifunzia, na mahudhurio ya wanafunzi wa kike yanakuwa bora zaidi kwa kuwa wanaweza kufika shuleni hata wakati wa hedhi.

Hata hivyo afisa huyo wa UNICEF amesema wanakabiliwa na kazi ngumu ya kuhakikisha kuwa fedha  zinaelekezwa katika ujenzi na ukarabati wa huduma za maji, usafi na kujisafi kwenye shule zote za msingi na sekondari.

Ripoti hii imelenga kupima utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs namba 4 linalohusu elimu na 6 la huduma za maji safi na kujisafi.