Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kigori 1 kati ya 3 kutoka familia maskini hawajawahi kwenda shule: UNICEF

Wasichana vigori wakiondoka shuleni kwenye mji wa Bol nchi Chad baada ya muda wa masomo
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wasichana vigori wakiondoka shuleni kwenye mji wa Bol nchi Chad baada ya muda wa masomo

Kigori 1 kati ya 3 kutoka familia maskini hawajawahi kwenda shule: UNICEF

Utamaduni na Elimu

Karibu msichana mmoja kigori kati ya watatu kutoka familia maskini kote duniani, hawajawai kwenda shule kwa mujibu ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF iliyozinduliwa leo wakati ambapo mawaziri wa elimu wanakusanyika kwenye mkutano wa dunia wa elimu kabla ya viongozi nao kukusanyika kwa mkutano wa kila mwaka kuhusu uchumi.

Umaskini, ubaguzi kwa misingi ya kijinsia, ulemavu, ubaguzi wa kikabila au lugha, umbali kutoka shuleni na miundo mbinu mibaya ni kati ya vikwazo ambavyo vinaendelea kuwazuia watoto maskini kupata elimu.

Nchi kila mahali zimewaangusha watoto maskini zaidi duniani, na kwa kufanya hivyo, zimejiangusha zenyewe, amesema mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore. Ikiwa matumizi kwenye elimu ya umma ni kidogo, wale maskini wana matumaini kidogo ya kujinusuru kutoka katika umaskini, kujifunza taaluma wanazohitaji kufanikiwa katika ulimwengu wa sasa na kuchangia katika uchumi wa nchi zao.

Wasichana wakiwa darasani mjini Bol nchini Chad
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wasichana wakiwa darasani mjini Bol nchini Chad

Kwa kuangalia nchi 42 zilizo na data, ripoti hiyo inaonyesha kuwa elimu kwa watoto kutoka  asilimia 20 ya familia tajiri hupewa karibu mara mbili ya ufadhili ambao asilimia 20 ya watoto kutoka familia maskini hupata.

Nchi kumi kutoka Afrika hukumbwa na changamoto kubwa zaidi katika ufadhili wa elimu ikiwa mara nne zaidi ya ufadhili kwa watoto matajiri ikilinganishwa na wale maskini.

Nchini Guinea na Jamhuri Ya Afrika ya kati CAR, ni nchi zenye viwango vya juu vya watoto wasio shuleni duniani, watoto matajiri hunufaika zaidi ikilinganishwa na ufadhili ambao watoto kutoka jamii maskini hupata.

Barbados, Denmark, Ireland, Norway na Sweden ndizo nchi pekee ambazo ugavi wa ufadhili wa elimu hufanyika kwa njia sawa kati ya watoto maskini na matajiri.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya nusu ya watoto wanoishi kwenye nchi za kipato cha chini na cha wastani hawawezi kusoma au kuelewa mambo kwa urahisi wanapomaliza shule ya msingi.