Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yashamirisha biashara mtandaoni:UNCTAD 

Matumizi ya mtandao kupitia simu ya rununu
Unsplash/Priscilla du Preez
Matumizi ya mtandao kupitia simu ya rununu

COVID-19 yashamirisha biashara mtandaoni:UNCTAD 

Afya

Janga la corona au COVID-19 limebadili mtazamo wa watu kuhusu kuelekea zaidi kwenye ulimwengu wa kidijitali kwa mujibu wa matokeo ya utafidi wa wateja uliofanywa hivi karibuni ya shirika la Umoja wa Mataifa la biashara na maendeleo UNCTAD. 

Utafiti huo uliofanyika kwa njia ya mtandao umeonesha kwamba mabadiliko ya tabia ya manunuzi mtandaoni huenda yakawa na athari za muda mrefu. 

Kwa mujibu wa UNCTAD utafiti huo “COVID-19 na biashara mtandaoni” uliohusisha wateja 3,700 katika nchi 9 zinazoendelea na zilizoendelea umedhihirisha kwamba janga la COVID-19 limebadili tabia ya manunuzi ya mtandaoni daima. 

Utafiti huo umetathimini jinsi gani janga hili lilivyobadili njia za wanunuzi kutumia biashara ya mtandaoni na suluhu za kidijitali na umejumuisha nchi za Brazil, China, Ujerumani, Italia, Jamhuri ya Korea, Urusi, Afrika Kusini, Uswisi na Uturuki. 

Matokeo ya utafiti 

Kwa mujibu wa utafiti huo kufuatia janga la COVID-19 zaidi ya nusu ya watu waliofanyiwa utafiti wamesema sasa wananunua vitu mtandaoni mara nyingi na wanategemea intaneti zaidi kwa kupata habari, taarifa kuhusu masuala ya afya na burudani. 

Wanunuzi kutoka nchi zinazoendelea utafiti huo unasema ndio waliofanya mabadiliko makubwa ya kuingia mtandaoni kununua vitu. 

“Janga la COVID-19 limeongeza kasi ya hulka ya kuingia kwenye ulimwengu wa kidijitali. Mabadiliko tunayofanya sasa yatakuwa na athari za muda mrefu wakati uchumi wa dunia ukianza kuchipuka tena.” Amesema Mukhisa Kituyi Katibu Mkuu wa UNCTAD. 

Ameongeza kuwa ongezeko la kasi la manunuzi mtandaoni duniani kote linadhihirisha uharaka wa kuhakikisha kwamba nchi zote zinaweza kuchukua fursa hizo zinatoletwa na ulimwengu wa kidijitali wakati dunia ikiondokana na janga la COVID-19. 

Manunuzi mtandaoni yapanda, fedha zinazotumika zapungua 

Utafiti huo uliofanywa kwa pamoja na UNCTAD na jumuiya ya biashara mtandaoni ya Uswisi Netcom wakishirikiana na kituo cha mtandao wa Habari cha Brazil NIC.Br na Inveno umeonyesha kwamba manunuzi mtandaoni yameongezeka kwa asilimia 6 hadi 10 katika bidhaa mbalimbali. 

Na walionufaika zaidi na biashara hizo ni makampuni ya teknolojia ICT, bidhaa vya kielektroniki, bidhaa za bustani, vitu vya kujitengenezea, makampuni ya madawa, elimu, samani, bidhaa za nyumbani na vipodozi na vifaa vya usafi binafsi na kujilinda. 

Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti wastani wa matumizi kwa mwezi kwa kila mnunuzi yamepungua . Wateja kutoka nchi zote zinazoendelea na zilizoendelea wameahirisha manunuzi ya kiwango kikiubwa cha fedha na kwa wale walio katika nchi zinazoendelea wakijikita zaidi na bidhaa muhimu na za lazima. 

Sekta zilizoathirika 

Ripoti pia imebaini kwamba sekta za utalii na usafiri zimeathirika sana kwa kupoteza pato kubwa ambapo kwa wastani manunuzi ya mteja yameshuka kwa asilimia 75 kwa bidhaa hizo za utalii na safari. 

Akizungumzia upande wa Brazil Alexandre Barbosa kutoka mtandao wa taarifa ncnhini Brazil NIC.br amesema “wakati wa janga la COVID-19 tabia ya matumizi ya mtandao nchini humo imebadilika kwa kiasi kikubwa huku watu wengi sasa wakitumia intaneti kununua mahitaji muhimu kama vile chakula na vinywaji, bidhaa za urembo na madawa.” 

Hata hivyo utafiti huo unasema ongezeko la manunuzi mtandaoni linatofautiana baina ya nchi , huku ongezeko kubwa likionekana Chjina na Uturuki huku nchi za Ujerumani na Uswis ongezeko si kubwa sana kwa sababu tayari watu wengi walikuwa wanajihusisha na biashara mtandaoni hata kabla ya COVID-19. 

Wanunuzi wakubwa mtandaoni 

Utafiti huo umebaini pia kwamba wanawake na watu wenye elimu ya juu wameongeza manunuzi yao mtandaoni kuliko watu wengine.  

Pia watu wenye umri wa kati ya miaka 25 na 44 ndio kundi lililoongeza zaidi manunuzi mtandaoni ikilinganishwa na makundi yenye umri mdogo. 

Kwa upande wa Brazil ongezeko kubwa limeshuhudiwa miongoni mwa watu walio hatarini zaidi na wanawake. 

Kwa upande wa uuzaji mzuri mtandaoni , utafiti umeonyesha kwamba wafanyabiashara wa China wamejiandaa vyema na wako vizuri zaidi katika kuuza bidhaa zao mtandaoni huku Afrika Kusini wakiwa na maandalizi kidogo sana. 

Makampuni ambayo yanatoa kipaumbele katika mikakati ya biashara mtandaoni wamejiandaa vyema kwa ajili ya kipindi baada ya COVID-19. Kuna fursa kubwa kwa viwanda na makampuni ambayo bado yanategemea watu kwenda kufanya manunuzi ana kwa ana kama bidhaa za walaji na makampuni ya madawa.” Amesema Yomi Kastro muasisi na mkurugenzi mtendani wa Inveon. 

Naye Rais wa NetComm ya Uswis Carlo Terreni amesema, “katika ulimwengu wa baada ya COVID-19 ukuaji usio sanjari wa biashara mtandaoni utaingilia mifumo ya kitaifa na kimataifa ya biashara za rejareja. Hii ndio sababu watunga sera lazima wachukue hatua Madhubuti kuwezesha biashara mtandaoni miongoni mwa wafanyabiashara wadogo na wa wastani, kuandaa kundi la wataalam wa ubunifu na kuvutia wawekezaji wa kimataifa wa biashara mtandaoni.” 

Makampuni ya kidijitali yazidi kuimatrika 

Kwa mujibu wa utafiti huo majukwaa ya kidijitali yanayotumika zaidi kwa mawasiliano ni Whatsapp, Instagram na Facebook Messenger, yote yakimilikiwa na Facebook. 

Hata hivyo Zoom na Microsoft Teams ni majukwaa yaliyofaidika sana kutokana na ongezeko la matumizi ya upigaji simu kwa njia ya video katika maeneo ya kazi. 

Nchini China majukwaa ya mawasiliano yanayoshika nafasi ya juu ni WeChat, DingTalk na Tencent Conference umesema utafiti huo. 

Mabadiliko yataendelea  

Matokeo ya utafiti huo yanapendekeza kwamba mabadiliko haya katika shughuli mtandaoni yanauwezekano wa kuendelea hata baada ya janga la COVID-19. 

Wengi walioshiriki utafiti huo hasa wale wa China na Uturuki wamdesema wataendelea kufanya manunuzi mtandaoni na kujikita Zaidi na bidhaa za muhimu hasa siku za usoni. 

Wameongeza kuwa pia wataendelea kusafiri ndfani hali inayoashiria athari za muda mrefu katika sekta ya utalii wa kimataifa.