Tufungue bandari zetu ili shehena za dawa na vifaa viweze kusaidia kukabili COVID-19 – UNCTAD

25 Machi 2020

Wakati nchi duniani zinaendelea kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, Umoja wa Mataifa umesema sekta ya usafirishaji majini ina dhima muhimu katika hatua dhidi ya janga hilo.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema hayo leo kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake mjini Geneva, Uswisi.

Dkt. Kituyi amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa takribani asilimia 80 ya shehena za biashara duniani husafirishwa kwa meli na shehena hizo ni pamoja na vifaa muhimu wa vya tiba vinavyohitajika zaidi hivi sasa, chakula, nishati, malighafi na vifaa vingine muhimu.

“Serikali zote zinapaswa kuruhusu kuendelea kwa sekta ya usafirishaji majini kwa kuwezesha meli za kibiashara kutia nanga kwenye bandari zao na kusaidia pia wafanyakazi hao wa meli kubadilishana zamu zao na huu ni wito ambao unapaswa kusikilizwa,” amesema Dkt. Kituyi.

Amekumbusha kuwa katika zama za sasa za janga la COVID-19, ni muhimu kuliko wakati wowote ule kuendeleza mnyororo wa usambazaji bidhaa na kuruhusu kuendelea kwa biashara kupitia usafirishaji majini.

“Hii ina maana bandari zifunguliwe na watendaji wa meli wafanye kazi zao bila vikwazo, vituo vya mpito viandaliwe kwa kuwa nchi zisizo na bandari zinahitaji kupata vyakula na dawa kupitia bandari za nchi jirani,”  amesisitiza Katibu Mtendaji huyo wa UNCTAD.

Amekumbusha kuwa katika kukabiliana na janga la sasa la ugonjwa wa virusi vya Corona, usafirishaji wa shehena za misaada ya kibinadamu pamoja na vifaa vya matibabu na dawa baina ya nchi utaongezeka kwa kiasi kikubwa na kwamba, “vizuizi vya kibiashara na usafirishaji mipakani vinaweza kukwamisha misaada na usaidizi wa kiufundi unaohitajika.”

Ametoa wito kwa viongozi wa kundi la nchi 20, G20 ambao wanakutana wiki hii kwa njia ya video kujadili COVID-19, kupatia kipaumbele wito wa tasnia ya usafirishaji majini ya kutaka bandari ziwe wazi ili usafirishaji wa shehena za mizigo na ubadilishanaji wa watendaji melini uendelee.

Je mabaharia wanakumbwa na vikwazo gani wakati wa COVID-19?

Kutokana na mlipuko wa ugonja wa virusi vya Corona, mabaharia wanakabiliwa na uchunguzi mkubwa katika bandari mbalimbali.

Dkt. Kituyi amesema kuwa, “bandari nyingi zimeweka kanuni za taifa husika, vikwazo na karantini vikizuia kuwafikia mabaharia melini. Baadhi ya kampuni zimesitisha ubadilishanaji wa mabaharia melini ili kuzuia makaribiano.”

Ni kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu huyo wa UNCTAD amesema kuwa huku kanuni muhimu za kiafya zikifuatwa, bandari zinapaswa kuona mabaharia kuwa ni watendaji muhimu na pindi wanapoingia au kutoka melini wapatiwe unafuu ule ule unaopatiwa wafanyakazi wa kwenye ndege na wale wa afya  kwa kuwa kila mwezi wafanyakzi 100,000 wa meli wanapaswa kubadilishana zamu za kazi.

Amegeukia pia wafanyakazi wa bandari akisema nao pia wako hatarini kuambukizwa COVID-19 hivyo bandari nazo zijiandae kwa kuwa hivi sasa idadi kubwa hazina maandalizi ya kutosha iwapo mfanyakazi anaugua ugonjwa huo.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter