Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usimamizi wa data ni muhimu ili biashara mtandao inufaishe wote- Amina 

Biashara mtandaoni inasaidia bidhaa kama hizi zinazotengenezwa huko huko Manzini, Swaziland kuweza kupatikana hata kwa wahitaji barani Asia
FAO/Giulio Napolitano
Biashara mtandaoni inasaidia bidhaa kama hizi zinazotengenezwa huko huko Manzini, Swaziland kuweza kupatikana hata kwa wahitaji barani Asia

Usimamizi wa data ni muhimu ili biashara mtandao inufaishe wote- Amina 

Ukuaji wa Kiuchumi

Wiki ya biashara mtandao inayosimamiwa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo, UNCTAD ikiwa imeanza, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema wiki hiyo inatoa fursa ya kuangalia upya matumizi ya data na mifumo na majukwaa ya kidijitali kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Katika ujumbe wake wa wiki hii ya biashara mtandao, aliotoa kwa njia ya video, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina J. Mohammed amesema biashara mtandao ni fursa mpya ya kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 

Amesema, “madhara makubwa yatokanayo na janga la coronavirus">COVID-19 yako hatarini kuwa makubwa zaidi kutokana na vita ya Ukraine. Katika zama za sasa zisizo za kawaida, ushirikiano wa kimataifa na ubia ni muhimu sana.” 

Amesema Wiki ya Biashara mtandao mwaka 2022 inatoa fursa kwa nchi na wadau kukutana na kujadili fursa kubwa mpya ya kutumia data na mifumo ya kidijitali kufanikisha SDGs. 

Hata hivyo amesema, “ingawa maendeleo ya kidijitali yanawakilisha uthabiti mkubwa mzuri wa kutuwezesha kukabili mahitaji yetu ya maendeleo kwa njia mpya, pia yanakuja na changamoto.” 

UNCTAD inasema nchi zisizo na uwezo wa kugeuza data kwa ajili ya matumizi ya kiintelijensia au fursa za biashara kusongesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, zinakosa fursa bora. 

Ameonya kuwa bila kushughulikia changamoto hizo, maendeleo ya kidijitali yanaweza kupunguza imani ya umma kwa serikali, kuibua ukosefu wa usawa n ahata kuongeza pengo la kidijitali ikiwemo kwa misingi ya jinsia. 

Bi.  Mohammed amesema vile ambavyo data zinatumika itakuwa na athari katika kufanikisha SDGs, hivyo serikali lazima zishirikiane na kujadili jinsi ya kutumia data kwa maslahi ya umma na iwe bidhaa ya umma na si vinginevyo. 

Ametaka kuwepo kwa mbinu bunifu za kusimamia data na uchumi wa kidijitali ili kuwe na mgao sawa. 

Wiki ya Biashara Mtandao iliyoanza tarehe 25  mwezi huu itaendelea hadi tarehe 29 na maudhui ni Data na maendeleo ya kidijitali kwa ajli ya maendeleo.