Vita vinavyoendelea Mashariki mwa Ukraine ni mslaba mzito kwa wazee:OCHA 

6 Oktoba 2020

Vita vinavyoendelea Mashariki mwa Ukraine vimeongeza madhila kwa maelfu ya wazee na sasa janga la corona au COVID-19 imekuwa ni kama msumari wa moto juu ya kidonda. Mfuko wa msaada wa kibinadamu wa Ukraine unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa ndio mkombozi pekee kwa wazee hawa. 

Mashariki mwa Ukraine kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA watu nusu milioni hawakuwa na uhakika wa chakula hata kabla ya janga la COVIDI-19, na baada ya kuzuka janga hilo hali imekuwa mbaya zaidi hasa kwa wazee wanaoishi karibu na eneo la mapigano. 

Huyu ni Liudymyla Mykolayivna mmoja wa wazee hao akisema anaishi peke yake na anasumbuliwa na tatizo la miguu, anahitaji msaada ukiwemo wa kupata mahitaji muhimu kama makaa na hata chakula kwani hata kwenda sokoni ni shida.  

Kupitia msaada wa mfuko huo wa mfuko wa Umoja wa mataifa shirika la kusaidia wazee help age linaweza kumletea mahitaji muhimu kila mwezi na vifaa vingine vya lazima. Liudmyla anasema,“Kama isingekuwa msaada wa wahudumu hawa , sijui ningefanya nini, nilikuwa na hali mbaya sana kiafya, mwaka jana hata kwenda msalani ilikuwa tabu , kupata msaada wa choo hiki kinachohamishika imenisaidia sana.” 

Eugenia mmoja wa wafanyakazi wa kujitolea wa Help age anasema wakati huu wa COVID-19 wazee wa umri wa zaidi ya miaka 60 wamekwama majumbani na shirika lao linajitahidi kwa kila njia kuwasaidia hata kwa shughuli za nyumbani kama kuchota maji wanapokwenda kuwatembelea  

Victor Ivanovych anaishi na mkewe ambaye ni mzee pia na hata kutembea ni mtihani. “Kuzuka kwa virusi hivi kila kitu kimebadilika, bei za bidhaa zimepanda, hatujui tutawezaje kumudu nishati msimu huu wa baridi, mke wangu hawezi kutembea bila msaada nilikata kiegemeo cha kiti sasa anatumia kitako chake kutembea” 

Victor anasema nyumba yao ambayo iliharibiwa na vita haina maji inabidi aende kuchota kisimani, lakini wahudu wa msaada wanamsaidia kwenda kutafuta mkate na hata kumlipia bili ya umeme kila mwezi. 

Wazee hawa Liudymila na Viktor ni sehemu ndogo tu ya wazee walioathirika na vita Ukaraine na kilio chao kwa mola ni kumaliza vita hivi haraka iwezekanavyo. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud