Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Acheni kushambulia vituo vya afya Ukraine

Mwanamke mjamzito wa Ukraine ambaye aliondoka Odesa na mama yake na mwanaye wa kiume akipokea msaada wa vifaa vya msingi kutoka UNFPA katika kituo mjini Chișinău.nchini Moldova
© UNFPA Moldova/Adriana Bîzgu
Mwanamke mjamzito wa Ukraine ambaye aliondoka Odesa na mama yake na mwanaye wa kiume akipokea msaada wa vifaa vya msingi kutoka UNFPA katika kituo mjini Chișinău.nchini Moldova

Acheni kushambulia vituo vya afya Ukraine

Afya

Viongozi wa mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa  wametoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi yoyote dhidi ya vituo vya afya nchini Ukraine kwa kuwa kitendo hicho siyo tu kinaua na kusababisha majeruhi miongoni mwa wagonjwa na wahudumu wa afya, bali pia kinaharibu miundombinu ya afya na maelfu ya watu kushindwa kupata huduma hiyo muhimu wakati huu ambapo mahitaji yameongezeka.

Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Dkt. Natalia Kanem wa lile la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA na Dkt. Tedros Ghebreyesus wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO wametoa kauli hiyo kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa leo katika miji ya Geneva, Uswisi na New York, Marekani.

Viongozi hao wamesema mashambulizi dhidi ya watu walio hatarini zaidi kama vile watoto wachanga, watoto, wajawazito, wagonjwa na wahudumu wa afya ambao wanaweka maisha yao rehani kuhudumia wengine, ni kitendo cha ukatili uliovuka mipaka.

“Nchini Ukraine tangu kuanza kwa vita, mfumo wa WHO wa kufuatilia mashambulizi dhidi ya mifumo ya afya, umerekodi visa 31 vya mashambulizi. Vituo 24 kati ya hivyo viliharibiwa kabisa, ilhali magari 5 ya wagonjwa yaliharibiwa kabisa. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu 12, majeruhi 34 na kukwamisha uwezekano wa watu kupata huduma za afya,” imesema taarifa hiyo ya pamoja.

WHO inaendelea kuthibitisha taarifa zaidi, kwa kuwa mashambulizi yanaendelea licha ya wito wa kutaka ulinzi kwenye vituo vya afya.

Mtoto mchanga akipimwa uzito katika hospitali moja nchini Ukraine tarehe 7 mwezi Machi mwaka huu wa 2022
UNICEF/Andriy Boyko
Mtoto mchanga akipimwa uzito katika hospitali moja nchini Ukraine tarehe 7 mwezi Machi mwaka huu wa 2022

Mashambulizi yanaendelea licha ya huduma kuhitajika zaidi

Zaidi ya wajawazito 4,300 wamejifungua nchini Ukraine tangu kuanza kwa vita tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu na wajawazito wengine 80,000 wanatajirwa kujifungua katika miezi mitatu ijayo.

Vifaa vya matibabu,  Oksijeni pamoja na vile vinavyohitaijka kwa ajili ya wajawazito wanaojifungua na matatizo vinapungua.

“Mfumo wa afya Ukraine umezidiwa uwezo na iwapo utasambaratisha basi itakuwa ni janga,” wamesema viongozi hao wakitaka kila hatua ichukuliwe ili kuzuia janga hilo lisitokee.

Sheria za kibinadamu na haki za binadamu zizingatiwe

Viongozi hao wamesema sheria za haki za binadamu na kibinadamu lazima zizingatiwe na ulinzi wa raia upatiwe kipaumbele.

"Wadau wetu  na wafanyakazi wa huduma za afya lazima wapatiwe usalama ili waweze kuendelea kutoa huduma zao kwa usalama, huduma kama vile chanjo dhidi ya COVID-19, Polio, na usambazaji wa huduma za afya nchini kote Ukraine." wamesisitiza viongozi hao.

UNFPA, UNICEF na WHO kwa upande wao wanaendelea kushirikiana na wadau ili kuimarisha huduma hizo na ziweze kukidhi mahitaji.

Wametaka pia sitisho la mapigano ikiwemo kuondolewa vikwazo vyote ili wananchi waweze kufikiwa popote pale walipo na misaada ya kibinadamu na zaidi ya yote wamesema “kumaliza mzozo huo kwa amani nchini Ukraine ni jambo linalowezekana.”