Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita imesababisha uhaba wa Oksijeni Ukraine ni muhimu kuwafikia wanaoihitaji:WHO

Madaktarim wakimuwekea hewa ya oksijeni mgonjwa wa COVID-19 katika hospitali ya Kramatorsk Ukraine
© UNICEF/Evgeniy Maloletka
Madaktarim wakimuwekea hewa ya oksijeni mgonjwa wa COVID-19 katika hospitali ya Kramatorsk Ukraine

Vita imesababisha uhaba wa Oksijeni Ukraine ni muhimu kuwafikia wanaoihitaji:WHO

Amani na Usalama

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO leo limetoa rai ya kuhakikisha huduma ya Oksijeni inawafikia mamia ya watu wanaoihitaji haraka nchini Ukraine ili kuokoa maisha yao.

Katika taarifa ya pamoja ya mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus na mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Dkt. Hans Henri P.Kluge iliyotolewa mjini Geneva Uswis wamesema vita vimesababisha uhaba wa huduma hiyo muhimu na kwamba sasa wanashirikiana na wadau ili kuweka utaratibu salama wa kusafirisha huduma hiyo kupitia Poland.

Hata wakati wa vita afya iwe kipaumbele

Viongozi hao wa WGHO wamesisitiza kwamba “Wakati huu wa janga la Ukraine, afya lazima ibaki kuwa kipeumbele cha kwanza cha hatua za msaada wa kibinadamu, na mifumo ya afya na vituo viendelee kulindwa, kufanya kazi, kuwa salama, huduma za matibabu kupatikana kwa wote wanaohitaji, na wafanyikazi wa afya walindwe ili waendelee kuokoa maisha.”

Wameongeza kuwa na hilo lazima lijumuishe utoaji salama na unaotegemewa wa vifaa muhimu vya matibabu, ikiwemo vifaa vya kuokoa maisha vya oksijeni, ambavyo ni muhimu kwa wagonjwa walio na hali mahtuti, pamoja na wale walio na COVID-19 ambao idadi yao ni 1,700 hospitalini hivi sasa, na wale walio na magonjwa mengine hatari kuanzia watoto wachanga hadi wazee yanayotokana na matatizo ya ujauzito, kujifungua, magonjwa ya muda mrefu, majeraha na kiwewe.

Muhudumu wa afya akumuhudumia mgonjwa wa COVID-19 katika hospitali ya Kharkiv Ukraine
© UNICEF/Evgenij Maloletka
Muhudumu wa afya akumuhudumia mgonjwa wa COVID-19 katika hospitali ya Kharkiv Ukraine

“Hali ya uhaba wa usambazaji wa oksijeni inakaribia kiwango cha hatari sana nchini Ukraine. Malori hayawezi kusafirisha usambazaji wa oksijeni kutoka kwenye kituo cha uzalishaji hadi hospitali kote nchini, pamoja na mji mkuu wa Kyiv. Hospitali nyingi zinaweza kumaliza akiba yao ya oksijeni ndani ya saa 24 zijazo. Baadhi tayari zimeisha. Hii inaweka maelfu ya maisha ya watu hatarini.” Wamesema madaktari hao.

Zaidi ya hayo, wamesema watengenezaji wa jenereta za oksijeni za kimatibabu katika maeneo kadhaa pia wanakabiliwa na uhaba wa kemikali ya zeolite, bidhaa muhimu, hasa inayoagizwa kutoka nje ya nchi ili kutoa oksijeni salama ya matibabu. 

Uingizaji salama wa zeolite kutoka nje ya Ukraine kwa ajili ya vituo vya utengenezaji wa oksijeni pia unahitajika.

Hatari kubwa kwa wagonjwa

Hali hii kwa mujibu wa WHO inazidisha hatari kwa wagonjwa, huduma muhimu za hospitali pia zinahatarishwa na uhaba wa umeme na magari ya kubeba wagonjwa ziko katika hatari ya kukumbwa katika mzozo huo.

Katika miaka ya hivi majuzi, kwa msaada wa WHO, Ukraine ilikuwa imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo yake ya afya chini ya mpango kabambe wa mageuzi ya afya. 

Hii ni pamoja na uongezaji wa haraka wa uwezo wa tiba ya oksijeni kwa wagonjwa mahtuti wakati wa janga la COVID-19. 

Kati ya vituo vya afya zaidi ya 600 kote nchini vilivyotathiminiwa na WHO wakati wa janga hilo, karibu nusu vilisaidiwa moja kwa moja kwa vifaa, ujuzi wa kiufundi na uwekezaji wa miundombinu, kuwezesha mamlaka ya afya kuokoa mamia ya maelfu ya maisha ya watu.

Maendeleo haya sasa yako katika hatari ya kusambaratishwa wakati kutokana na mzozo wa sasa.

WHO inasaidia mamlaka za afya kutambua mahitaji ya haraka ya usambazaji wa hewa ya oksijeni nchini, ikikadiria ongezeko la asilimia 20% hadi 25% ya mahitaji ya hapo awali kabla ya mzozo kuongezeka wiki iliyopita.

Licha ya changamoto zinazoletwa na hali ya sasa, WHO inajitahidi kuhakikisha usambazaji wa vifaa vya matibabu vinavyohusiana na hewa ya oksijeni na vifaa vya matibabu ya majeraha.

Ili kufanikisha hili, WHO inaangalia kikamilifu suluhu za kuongeza vifaa ambavyo vinaweza kujumuisha uagizaji wa mitungi ya hewa ya oksijeni kutoka kwwenye  mitandao ya kikanda. 

Vifaa hivi vinahitaji usafiri salama, kupitia Poland. “Ni muhimu kuhakikisha kwamba vifaa vya matibabu vinavyookoa maisha ikiwa ni pamoja na hewa ya oksijeni vinawafikia wale woten wanaohitaji kwa usalama.”.