Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manusura wa COVID-19 waandika barua kudai chanjo yenye utu, isiyojali kipato cha mtu

Adrien Bali, mwenye umri wa miaka 56 akizungumza katika hospitali ya Mtakatifu Joseph mjini Kinshasa, nchini DRC baada ya kupona COVID-19.
UNICEF VIDEO
Adrien Bali, mwenye umri wa miaka 56 akizungumza katika hospitali ya Mtakatifu Joseph mjini Kinshasa, nchini DRC baada ya kupona COVID-19.

Manusura wa COVID-19 waandika barua kudai chanjo yenye utu, isiyojali kipato cha mtu

Afya

Manusura wa ugonjwa wa Corona au COVID-19 kutoka mataifa 37 duniani  ni miongoni mwa watu waliopaza sauti kutaka chanjo dhidi ya ugonjwa huo itakapopatikana iweze kumfikia kila mtu popote pale alipo bila kujali hali yake ya kiuchumi au kijamii na isiwe na hataza.

Taarifa iliyootolewa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya Ukimwi, UNAIDS, imesema kuwa manusura hao wamepaza sauti yao kwenye barua ya wazi iliyoelekezwa kwa viongozi wa kampuni za dawa ikitoa wito kwa chanjo yenye utu na inayojali watu na isiyo na hataza..

Barua hiyo imeandikwa ikiwa ni siku moja kabla ya mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu janga la Corona utakafaonyika New York Marekani na mtandaoni tarehe 30 mwezi huu wa Septemba.

“Waliotia saini barua hiyo ni pamoja na manusura 242 wa COVID-19 kutoka Afrika Kusini, Finland, New Zealand na Brazil Halikadhalika kuna watu 190 katika nchi 46 ambao wamepoteza ndugu na jamaa zao kutokana na virusi hivyo vya Corona ilhali wengine 572 wana hali dhoofu za kiafya, ikimaanisha kuwa wako hatarini kuugua zaidi iwapo wataambukizwa virusi vya Corona,” imesema taarifa hiyo ya UNAIDS.

Wananchi wa Sudan Kusini katika soko la Konyo Konyo mjini Juba wakijisomea taarifa kuhusu COVID-19 baada ya kupatiwa barakoa za kitambaa.
© UNICEF/Bullen Chol
Wananchi wa Sudan Kusini katika soko la Konyo Konyo mjini Juba wakijisomea taarifa kuhusu COVID-19 baada ya kupatiwa barakoa za kitambaa.

Barua inasema, “baadhi yetu tumepoteza wapendwa wetu kutokana na gonjwa hilli hatari Baadhi yetu tumeponea chupuchupu. Baadhi yetu tunaendelea kuishi kwa hofu kubwa ya kwamba tukiambukizwa tu huu ugonjwa, basi ndio mwisho wa maisha yetu. Hatuoni uhalali wowote wa kwa nini faida yetu au ukiritimba wenu unaweza kumaanisha mtu yeyote anaweza kupitia hiki tunachopitia.”

Barua hiyo inaelezea kampuni za kutengeneza dawa kama kampuni zinazoendelea na shughuli zao kama kawaida, zikitetea ukiritimba wao na kukataa kubadilishana tafiti na ujuzi na kutoa wito kwa viongozi wahakikishe kuwa chanjo dhidi ya COVID-19 na tiba vinamfikia kila mtu anayehitaji kwa kuzuia ukiritimba na uzuiaji wa kubadilishana ufahamu wa utengenezaji wa chanjo hiyo.
Ukiritimba wa kampuni za dawa unamaanisha kuzuia uzalishaji wa chanjo fanisi kwa kampuni ndogo, kuzuia uzalishaji wa chanjo kwa kiwango kikubwa kinachotakiwa kukidhi mahitaji duniani.
Ni kwa mantiki hiyo barua hiyo inataka kampuni zitoe leseni ya teknolojia ya chanjo hiyo na hakimiliki kwa mfumo wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, wa kubadilishana teknolojia au (C-TAP).

Alichoandika mmoja wa manusura wa COVID-19

Mmoja wa waliotia saini ni Dilafruz Gufurova mwenye umri wa miaka 43 kutoka Tajikistan ambaye amesema, “mimi na mume wangu tuliugua Corona. Tulijitegemea wenyewe kwa kuwa hospitali zilikuwa zimejaa. Ilikuwa wakati mgumu sana kupata dawa sahihi. Mimi ni mama wa watoto wanne, nilikuwa nahofia kuwaacha peke yao katika dunia hii iwapo lolote lile lingalitokea kwangu. Sababu ya kutia saini barua hii ni kusaidia wengine wapate chanjo. Si watu wote duniani kote wanaweza kupata chanjo, kwa kuwa hawawezi kumudu gharama. Wana uwezo mdogo kabisa hata kukimu mahitaji yao ya kila siku.”

Uandishi wa barua hiyo uliratibiwa na kikundi cha ushawishi wa kupatikana kwa chanjo yenye utu, People's Vaccine Alliance, chombo ambacho ni ushirika wa mashirika na wanaharakati walioungana kuona chanjo ya COVID-19 inapatikana kwa kila mtu.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima, akizungumzia umuhimu wa chanjo amesema, “wakati wa UKIMWI  matibabu yalipopatikana, watu matajiri katika nchi tajiri walirejea katika afya yao na mamilioni ya watu katika nchi zinazoendelea waliachwa wafe. Katu tusirudie kosa hilo pindi chanjo dhidi ya COVID-19 itakapopatikana. Haki ya afya ni haki ya binadamu, haipaswi kutegemea uwezo wa fedha kwenye mfuko, rangi ya mtu. Chanjo inapaswa kuwa kitu cha maslahi ya kila mtu.”

Barua hiyo imeandikwa wakati huu ambapo idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na COVID-19 duniani kote imevuka milioni moja.