Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hebu tufutieni kabisa madeni LDCs ili tujikwamue vyema baada ya COVID-19- Malawi

Rais Lazarus chakwera wa Malawi (kwenye skrini) akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 kwa njia ya video kutoka Malawi.
UN/Eskinder Debebe
Rais Lazarus chakwera wa Malawi (kwenye skrini) akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 kwa njia ya video kutoka Malawi.

Hebu tufutieni kabisa madeni LDCs ili tujikwamue vyema baada ya COVID-19- Malawi

Afya

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amehutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo akisema kuwa mjadala huo unafanyika wakati ambao dunia imegubikwa na janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19, na hali ikiwa mbayá zaidi kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Malawi.
 

Katika hotuba hiyo kwa njia ya video kutoka Lilongwe, Malawi, Rais Chakwera amefafanua kuwa Malawi imeathirika zaidi pamoja na nchi nyingine zisizounganishwa na baharí kwa sababu ya kukosa ushindani kwenye biashara, gharama kubwa za tozo la ushuru na kwamba COVID-19 imekwamisha harakati za kujiendeleza kiuchumi na kijamii.

Rais Chikwera ambaye pia ni Mwenyekiti wa kundi la nchi zinazoendelea, LDCs, amesema kwa mwelekeo wa sasa kuna hatari kubwa ya nchi hizo kushindwa kulipa madeni.

Hivyo amesema, “tunatambua uamuzi wa Benki ya Dunia, shirika la fedha duniani, IFM na shirika la maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi, OECD na wadau wengine wengi wa kusitisha kwa muda ulipaji madeni kwa LDCs. Lakini kwa kutambua jinsi janga hili litaendelea kuwepo kwa muda mrefu na madhara yake zaidi, tunaomba na tunatumaini kufutwa kabisa kwa madeni, na pia kuongezwa muda wa sitisho la kulipa madeni.”

Huko Muona, Wilaya ya Nsanje (Malawi Kusini) walengwa wanaulizwa kuosha mikono na sabuni kabla na baada ya kupata vifaa vyao
WFP/Badre Bahaji
Huko Muona, Wilaya ya Nsanje (Malawi Kusini) walengwa wanaulizwa kuosha mikono na sabuni kabla na baada ya kupata vifaa vyao

Rais Chikwera amesema hiyo itawezesha nchi za LDCs kukwamuka kutokana na janga hili kiendelevu zaidi
Amegusia pia suala la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs akisema kuwa Malawi imejikita katika kutekeleza malengo hayo kwa kujumuisha pande zote hata wakati huu wa janga la Corona.

“Tunajivunia kuwa mwezi Julai mwaka huu tulishiriki katika tathmini ya hiari ya utekelezaji wa SDGs katikati ya janga la Corona. Tunaomba kuungwa mkono zaidi na wadau wetu,” amesema Rais Chikwera.

Uchaguzi wa Malawi

Ametumia pia hotuba hiyo ya dakika 18 na nusu,  kuelezea kuwa ni hotuba yake ya kwanza tangu kuchaguliwa na kuapishwa kuwa Rais mwezi Juni mwaka huu.

“Uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na haki na kudhihirisha misingi ya demokrasia ya Malawi na hata kipindi cha makabidhiano kutoka kwa mtangulizi wangu kimekwenda kwa amani,” amesema Rais Chakwera.

Marekebisho ya Baraza la Usalama

Rais huyo wa Malawi akaeleza kuwa wanatambua marekebisho yanayofanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye chombo hicho chenye wanachama 193.

Hata hivyo wana hofu na hali ya marekebisho ya Baraza la Usalama, hivyo “Malawi inasisitiza marekebisho ya haraka ya Baraza la usalama na yawe na uwakilishi thabiti wa Afrika kwa mujibu wa tamko la Zhulweni la Muungano wa Afrika. Tunataka viti viwili vyenye kura turufu na viti vitano visivyo vya kudumu kwa Afrika. Tunahitaji Umoja wa Mataifa unaokidhi mahitaij ya Afrika kwenye ulinzi wa amani na hiyo inawezekana iwapo  Afrika inashiriki katika kufanya maamuzi hayo. Kwa kuzingatia migogoro inayokumba bara la Afrika hivi sasa na kukwamisha maendeleo yake, marekebisho hayo yamechelewa mno.”