Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekebisho ya Baraza la Usalama ni suala la dharura- Rais Ramaphosa

Rais wa Afrika Kusini Matamela Cyril Ramaphosa (kwenye skrini) akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video.
UN/Eskinder Debebe
Rais wa Afrika Kusini Matamela Cyril Ramaphosa (kwenye skrini) akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video.

Marekebisho ya Baraza la Usalama ni suala la dharura- Rais Ramaphosa

Afya

Miaka 75 iliyopita, Umoja wa Mataifa ulianzishwa ili kuiingiza dunia katika zama mpya za amani, na kuleta matumaini ya zama mpya za ushirikiano wa kimataifa baada ya nyakati za giza zaidi duniani, ndivyo alivyoanza hotuba yake Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kwa viongozi wa nchi na serikali wanachama wa Umoja wa Mataifa hii leo.
 

Akihutubia kwa njia ya video kutoka Pretoria Afrika Kusini, Rais Ramaphosa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, AU amesema baada ya vita kuu ya pili ya dunia, “sasa dunia iko katika janga lingine la virusi vya Corona.”
COVID-19 hadi sasa imesababisha vifo vya watu takribani milioni 1 kati ya milioni 4.5 waliothibitishwa kuugua gonjwa hilo ambalo  hadi sasa halina chanjo wala tiba, zaidi ya mtu kujikinga kwa njia mbalimbali ikiwemo kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa sababu au vitakasaji.
“Lakini kama vile ambavyo waasisi wa Umoja wa Mataifa walisimama kidete kwa maslahi ya wote, nasi pia tunaweza kuungana na kukabili kitisho hiki kikubwa,”  amesema Rais huyo wa Afrika Kusini.
Ameongeza kuwa hatua zilizochukuliwa hadi sasa zinaonesha kile kinachoweza kufanikiwa pindi jamii ya kimataifa ikifanya kazi kwa urafiki na mshikamano.

“Iwapo tunataka kujenga mustakabali mmoja na jumuishi baada ya COVID-19 basi ni mshikamano huu ambao unapaswa kuhimili,” amesisitiza Bwana Ramaphosa akinukuu maneno ya Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandele aliyesema kuwa, “ni mshikamano wa binadamu, kujali wengine ambavyo vinapaswa kuwa kitovu cha maadili ambayo tunayaishi.”

Livhuwani Hellen Dzibana, mfanyakazi wa kijamii nchini Afrika Kusini akizungumza na mmoja wa wateja wake.
UNICEF VIDEO
Livhuwani Hellen Dzibana, mfanyakazi wa kijamii nchini Afrika Kusini akizungumza na mmoja wa wateja wake.

AFRIKA na COVID-19

Bara la Afrika lilichukua hatua za haraka na fanisi kukabili Corona na kwamba hivi sasa kuna mkakati wa kibara wa kutokomeza janga la Corona, mkakati unaoongozwa na jumuiya za kiuchumi za kikanda.

Amesema kuwa Muungano wa Afrika ulianzisha mfuko wa kukabili COVID-19 sambamba na jukwaa la kusambaza vifaa vya matibabu barani Afrika ili kuhakikisha kuwa kila nchi ina vifaa muhimu vinavyohitajika.

Hata hivyo amesema kuwa janga la Corona linarudisha nyuma maendeleo kwa kuwa rasilimali zimeelekezwa katika kutokomeza janga hilo badala ya kwenye miundombinu ya afya, elimu na mawasiliano.

Kwa mantiki hiyo amekumbusha umuhimu wa kuanzishwa kwa makubaliano mapya ya kusaidia kuwepo kwa mfumo mahsusi wa kusaidia nchi za Afrika kujikwamua baada ya COVID-19.

“Hii itasaidia nchi za Afrika siyo tu kupunguza athari za kiafya kutokana na COVID-19, bali pia kusaidia kurejea katika jukumu adhimu la kujenga chumi zetu zilizoporomoshwa,” amesema Rais huyo wa Afrika Kusini.

AU na Baraza la Usalama

Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Afrika ametumia pia hotuba yake kukumbusha kuwa aina ya ujumbe katika Baraza la Usalama hauakisi taswira halisi ya ulimwengu wa sasa.

Amesema Umoja wa Mataifa unapoadhimisha miaka 75, “tunarejelea wito wetu wa kutaka wigo mpana wa uwakilishi kutoka nchi za Afrika katika Baraza la Usalama, na hoja hii izingatiwe kidharura katika mashauriano baina ya serikali.”

Rais Ramaphosa amesisitiza kuwa ni kwa kupitia Baraza lililorekebishwa na jumuishi la usalama nidpo kwa pamoja nchi wanachama zitaweza kutatua mizozo iliyodumu miaka nenda miaka rudi duniani.