Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa ndani na wa kimataifa umetusaidia-Rais Farmajo wa Somalia 

Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo, Rais wa Seikali kuu ya Jamhuri ya Somalia (Picha ya maktaba)
UN Photo/Laura Jarriel
Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo, Rais wa Seikali kuu ya Jamhuri ya Somalia (Picha ya maktaba)

Ushirikiano wa ndani na wa kimataifa umetusaidia-Rais Farmajo wa Somalia 

Afya

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo hii leo akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video iliyorekodiwa, amesema wanaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa na wadau wengine katika masuala mbalimbali ili kutengeneza mstakabali mzuri kwa watu wa Somalia. 

Rais Farmajo kama walivyofanya marais wengine waliotangulia, hakuacha kuanza kwa kuzungumzia namna janga la virusi vya corona vilivyoathiri nchi nyingi ikiwemo Somalia lakini wamechukua hatua kupambana na ugonjwa huo. 

“Nchini Somalia, serikali yetu na watu wamefanya kazi kwa karibu ili kupunguza athari mbaya za janga la COVID-19. Kama serikali nyingi ulimwenguni, tuliipa kipaumbele afya za raia wetu na tukafanya kadri iwezekanavyo kuokoa maisha. Kupitia utoaji wa moja kwa moja wa matibabu na habari za uhakika na zinayofaa za afya ya umma, serikali yetu ilijitahidi sana kuweka watu salama iwezekanavyo. Maambukizi ya COVID 19 ambayo yalikuwa yanaongezeka haraka katika hatua za mwanzo za janga hilo, zimeshuka kwa kasi kutokana na hatua za haraka za serikali yetu.” Ameeleza Rais Farmajo. 

Rais huyo akisisitiza na kuonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa amesema mafanikio walioyafikia katika kupambana na COVID-19 yasingewezekana kama si ushirikiano thabiti katika ya serikali, wananchi na washirika wao wa kimataifa hata hivyo, “kufanikiwa kwa juhudi zetu nchini Somalia haimaanishi kwamba hatujasumbuliwa. Kulingana na takwimu rasmi, zaidi ya Wasomali 3,000 waliambukizwa na virusi hivyo na karibu 100 walipoteza maisha yao kwa sababu hiyo. Wengi zaidi ambao waligunduliwa walilazimika kuishi na maumivu na mateso ya COVID 19 na wengine bado wanaendelea kuwa katika mazingira magumu kutokana na udhaifu wa mifumo ya afya na miundombinu ya Somalia.” 

Kuhusu uchaguzi 

Kwa upande wa maendeleo ya watu na demokrasia, Rais Farmajo amesema Somalia inafanya kazi na kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kuunda mstakabali mzuri kwa Somalia na ulimwengu.   

“Tunaongoza katika kupeleka maendeleo kwa watu wetu na kufanya kazi na washirika wetu muhimu wa kimataifa kuhakikisha tunajenga tena Somalia yenye demokrasia, inayojumuisha na yenye uchumi. Licha ya changamoto za COVID-19, bado tunafanya kazi kwa bidii kufanya uchaguzi wa kitaifa jumuishi ambapo watu wa Somalia wanaweza kuamua maisha yao ya baadaye. Tumejitolea kabisa kukuza utamaduni thabiti wa demokrasia na utawala unaowajibika ambao unawatumikia watu wa Somalia kwanza kabisa.” Amesisitiza. 

Kuhusu usalama 

Rais huyo wa Somalia amesema pia wanafanikiwa katika kuishinda hatari ya ugaidi wa kimataifa akisema hiyo ni kutokana na juhudi za vikosi jasiri vya Somalia kwa kushirkiana na AMISOM. 

“Nina imani na juhudi za serikali yetu na kuendelea kuungwa mkono na washirika wetu muhimu wa kimataifa, Somalia sio tu itakabiliana na COVID 19 lakini itachangia vyema kwa juhudi za pande zote zinazohitajika kuUfanya ulimwengu kuwa mahali pazuri, penye mnepo zaidi na sawa kwa wote.” Amesema Bwana Farmajo.